Na Kija Elias, Moshi
Wakati serikali ikihaha kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu, katika hali ya kusikitisha, mwalimu wa skuli ya sekondari ya Muungano, Rashid Ndoile (30) anashilikiwa na polisi mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kufumaniwa akifanya ngono na mwanafunzi gesti moja iliyopo mji mdogo wa Himo.
Tukio hilo la kusikitisha ambalo limethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita, lilitokea Oktoba 3 saa tano asubuhi, katika nyuma ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Kilimanjaro.
Alisema wawili hao walifumaniwa na wazazi wa mwanafunzi.
Alisema siku ya tukio mwalimu huyo alionekana na wazazi wa mwanafunzi huyo, akipita na pikipiki huku akiwa amembeba mwanafunzi huyo, hali ambayo iliibua mashaka na kuamua kumfuatilia.
Alisema baada ya wazazi kumfuatilia mwalimu huyo, waliwakuta chumbani katika gesti hiyo jambo ambalo liliwafanya watoe taarifa polisi na mwalimu huyo kukamatwa.
Alisema kwa sasa, mwalimu huyo anashikiliwa kituo cha polisi Himo kwa mahojiano zaidi na kwamba upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Wakati huo huo, mwalimu mmoja wa skuli ya sekondari ya Uparo, aliyefahamika kwa jina moja la Matanda,anadaiwa kufumaniwa na wanafunzi wa skuli ya msingi iliyopo jirani na skuli anayofundisha akifanya ngono na mwanafunzi wake wa kidato cha tatu katika kichaka karibu na skuli hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka baadhi ya wazazi wenye wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo iliyopo halmashauri ya wilaya ya Moshi Vijijini, mara baada ya kufumaniwa, tukio hilo lilimalizwa kimya kimya na mkuu wa skuli hiyo ambapo baadaye mwalimu huyo alihamishiwa skuli ya sekondari ya Langasani iliyopo eneo la TPC.
Ofisa Elimu wa sekondari halmashauri ya wilaya ya Moshi Vijijini, Dk. George Jidamva, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alikana kuzifahamu na kuahidi kufuatilia.