Na Mwanajuma Mmanga
Jumla ya watoto 81 wamezaliwa katika mkesha wa sikukuu ya Idd el Hajj katika hospitali ya Mnanzimmoja na Muembeladu.
Kati ya watoto hao, 61 wamezaliwa hospitali ya Mnazimmoja wakiwemo wanawake wakiwa 34, ambapo wawili walifariki dunia baada ya kuzaliwa wakati mama zao wakiwa njia kuelekea hospitali kwa ajili ya kujifungua.
Katika hospitali ya Muembeladu walozaliwa watoto 20 katika ya hao wanawake 8 na wanaume 12.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa hospitali ya Mnazimmoja, Hassan Makame, alisema watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito wa juu ni kilo 3.5 na uzito wa chini ni kilo 2.
Alisema watoto hao wako salama na hawana matatizo yoyote ya kiafya na kwamba wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Msaidizi Muuguzi Dhamana wa hospitali ya Muembeladu, Mgret Sylveter Tayari, alisema uzito wa watoto waliozaliwa hospitali hiyo ni baina ya kilo 4.2 na 3.
Akizitaja changamoto wanazokumbana nazo katika kuwahudumia mama wajawazito wakati wanapofika kituoni kujifungua ni pamoja na kuchelewa kufika hospitali wakisubiri waumwe na uchungu.
Aidha, alisema wengine wanatumia dawa za asili kuongeza uchungu hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha yao na watoto.
Aliitaka jamii kuhamasika kuvitumia vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.