Na Mwandishi wetu
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) leo kitazindua taarifa ya utafiti kuhusu kiwango cha unywaji pombe na ukatili wa kijinsia.
Taarifa ya utafiti huo inaonesha kiwango cha unywaji pombe, sababu zinazopelekea watu kunywa kupita kiasi, madhara, kiwango cha upatikanaji pombe, ufahamu kuhusu matumizi na uhusiano kati ya matumizi ya pombe na ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Kinondoni.
Kuna uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya pombe na tabia ya kufanya vurugu, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu Tanzania (TDHS) ya mwaka 2010, matokeo yalionesha wanawake ambao waume zao ni walevi wako katika hatari ya kufikwa na ukatili wa kihisia, kimwili au kingono mara mbili zaidi ya wanawake ambao waume wao hawanywi pombe.
Uzinduzi wa utafiti huo ni sehemu ya mradi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia unaotokana na matumizi ya pombe dhidi ya wanawake na wasichana, unaofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya IOGT wenye lengo la kujenga uelewa miongoni mwa jamii juu ya madhara yatokanayo na pombe ili kupambana na ukatili unaotokana na pombe.
Mradi wa IOGT una miaka mitatu ya mafanikio tangu umefanya kazi na TAMWA.