Mwandishi wetu na mitandao
WAKATI Zanzibar ikichukua juhudi kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini kwa kuwapima abiria wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege na bandarini, imebainika tiba ya mgonjwa mmoja wa Ebola ni dola za Marekani 315,000 sawa na shilingi milioni 520.4.
Hata hivyo, hakuna dawa mahasusi wala chanjo ya ugonjwa huo hatari ambao tayari umeanza kuingia nchini Uganda baada ya mtu mmoja kufariki kwa kupatwa na virusi vya homa ya Marburg, ambavyo vinashabihiana kwa sehemu kubwa na Ebola.
Badala yake madaktari katika kliniki zinazowahudumia wagonjwa wa Ebola wanamsaidia mgonjwa kwa kumuongezea maji, kupunguza shinikizo la damu, kumuwekea mashine ya oxygen, kumuongezea damu na kutibu magonjwa mengine nyemelezi.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, umegundua gharama kubwa za kuwatibu wagonjwa wa Ebola na upungufu wa wataalamu ni miongoni mwa sababu zinazopelekea nchi za Afrika kushindwa kudhibiti ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, ugonjwa huo unaweza kudhoofisha uchumi wa Afrika kwa sababu ya gharama kubwa za kuwatibu wagonjwa.
Shirika hilo limewanukuu wanasayansi wakisema kuwa kuna hatari kubwa ya ugonjwa huo kusambaa katika mataifa ya magharibi hasa Uingereza na Ufaransa kutokana na safari nyingi za ndege zilizopo kati ya nchi hizo na mataifa yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) halijazuia safari za ndege katika mataifa yaliyoathiriwa na ugonjwa huo badala yake imekuwa ikiyahamasisha mashirika ya ndege kuchukua tahadhari.
Mashirika ya Ndege ya Uingereza na Emirates, yamesimamisha safari zake katika nchi za Afrika Magharibi zenye visa vya Ebola.