Na Fatina Mathias, Dodoma
SHEREHE ya kukabidhiwa katiba inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, zitafanyika leo katika viwanja vya Jamuhuri mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Nchimbi, alisema tukio hilo la kihistoria litafanyika kuanzia saa sita mchana na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia.
Pamoja na viongozi hao, tukio hilo pia litahudhuriwa na Marais wastaafu wa Muungano na Zanzibar, viongozi wa kitaifa na watendaji wakuu, viongozi wakuu wastaafu, Maspika wastaafu, Mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa, taasisi za kidini, taasisi zisizo za kiserikali na wamiliki wa vyombo vya habari.
Alisema kutakuwepo na makundi mbalimbali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo ni pamoja na wafugaji, wakulima, wavuvi, wanawake, vijana, wazee, wachimbaji madini wadogo, walemavu na wasanii.
Aidha, alisema ulinzi na usalama utakuwepo na utaendelea kuwepo.