Na Mwanajuma Abdi, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imesema zoezi la ufangaji mitambo ya video conference ya kurahisisha mawasiliano na nchi za jirani na kimataifa bila ya kutumia gharama za kusafiri, limekamika katika Ofisi ya Rais Ikulu na mikoa minne ya Zanzibar.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa video conference, uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo ulijumuisha mikoa ya Mwanza, Rukwa, Pwani, Dodoma, Mtwara na Shinyanga, ambapo Waziri Mnyaa alizungumza moja kwa moja na mikoa hiyo kupitia video conference kwa kuonana ‘live’ kama wapo katika ukumbi wa mkutano na kufanyiana mahojiano.
Alisema mkandarasi tayari ameshakamilisha zoezi hilo visiwani Zanzibar, ambapo hatua zinazoendelea ni kuwapatia mafunzo watendaji wa serikali ili kuweza kuitimia katika kurahisisha mawasiliano.
Aidha, alisema serikali itahakikisha ifikapo Oktoba mwakani katika ofisi zote za halmashauri, wilaya, hospitali, vituo vya polisi zitaunganishwa katika huduma hiyo ili kurahisisha mawasiliano.
Alisema katika kuhakikisha matumizi ya Tehama yanakuwa kwa kasi hasa katika ofisi za serikali, wizara imefunga mitambo hiyo katika ofisi zote mbili ya Dar es Salaam na Dodoma, makao makuu ya mikoa 21 ya Tanzania Bara, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Tamisemi.
Alifahamisha huduma ya teknolojia ya video conference ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya serikali, ambapo utumiaji huo unaweza kuwasaidia viongozi au watendaji na watalaamu kufanya kazi kwa kushirikiana na kuwasiliana na wadau wengine katika sehemu zao za kazi bila ya kulazimika kusafiri kutoka sehemu moja kwenda kwengine.
Alisema ujenzi wa mkonge wa taifa wa mawasiliano unaotekelezwa na wizara yake, unasanifu mradi wenyewe, utekelezaji unafanywa kwa awamu tano, ambapo ya kwanza na ya pili zimekamilika na kutumika tokea mwaka 2012, ikiwa na jumla ya kilomita 7,560 ambao umechangia kuleta mageuzi makubwa katika matumizi ya Tehama nchini.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa mradi wa mafunzo kwa njia ya mtandao, Charles Senkondo, alisema teknolojia hiyo imeongeza kasi ya uchumi na kijamii, ambapo vituo zaidi ya 120 vimeunganishwa duniani, ambapo nchi nyingi za Afrika bado huduma hiyo lakini kwa Tanzania imewahi.