Na Madina Issa
Mkuun wa Wilaya ya kati Unguja, Vuai Mwinyi, amewataka wananchi kuvitumia vituo vya afya na hospitali na kuacha tabia ya kutumia dawa za miti shamba.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika kilele cha siku ya uoni duniani katika kituo cha afya Mwera wilaya ya kati Unguja.
Alisema hivi sasa jamii imeonekana kutokuwa na muamko wa kuwapeleka watoto wao vituo vya afya, jambo ambalo husababisha kupata ugonjwa wa macho.
Alisema watu milioni 56 wamepofuka kati yao asilimia 80 ni kutoka nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar.
Alisema wataalamu wa maradhi na tiba ya macho kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na taasisi mbalimbali wako mbioni kupambana na tatizo hilo ingawa bado mafanikio ni madogo.
Aliishauri jamii kuwapeleka watoto wao vituo vya afya na hospital kwa ajili ya kupatiwa matibabu mapema.
Mapema Mratibu wa huduma za macho vijijini, Dk. Issa Muhsin Burhani, alisema ujumbe wa mwaka huu unalenga kupunguza au kutokomeza kabisa matatizo ya macho yakiwemo upofu.
Nae Mratibu wa huduma za macho Zanzibar, Dk. Fatma Juma Omar, alisema siku ya uoni duniani huadhimishwa kila ifikapo Alhamis ya pili ya mwenzi Oktoba kila mwaka.