Na Kija Elias, Tanga
Mkaguzi wa skuli za sekondari manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mtenguzi Kidyamakuo, ametangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Handeni mkoani Tanga, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Jimbo hilo kwa sasa linashikiliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdhalla Kigoda.
Alisema atagombea nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA).
Alisema amefikia huo uamuzi kwa lengo la kuharakisha masuala ya kimaendeleo ambayo amedai yanasuasua.
“Jimbo hili limekuwa na wabunge mbalimbali kwa zaidi ya miaka 20 sasa lakini hakuna maendeleo ya haja ambayo wananchi wake wanaweza kujivunia,” alisema.
Alisema moja wapo ya changamoto ambazo atalishughulikia ni pamoja na miundombinu ya barabara na maji ambayo alisema zimekuwa zikikwamisha wananchi katika juhudi zao za kujikwamua kiuchumi.
“Ukija kwa huduma za afya wananchi wa jimbo hili wanalazimika kutembea zaidi kilomita 30 kufuatialia huduma hizo huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto, wanawake na wazee,” aliongeza.
Alivitaja baadhi ya vijiji ambavyo vinakabiliwa na changamoto hizo kuwa ni Kwa Magoma, Msente, Tilibe, Muumbiri, Mzindu, Kwa Mkono na Kwedikwazu.