Na Hassan Silayo, Maelezo
Taasisi ya tiba ya mifupa, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu (MOI) imeendelea kuwa nguzo muhimu nchini katika utoaji wa huduma za tiba na upasuaji.
Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo, Patrick Mvungi, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema MOI imesaidia kuokoa maisha ya zaidi ya asilimia 95 ya Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wangeweza kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.
“MOI kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuokoa maisha ya Watanzania kwa zaidi ya asilimia 95 kutokana na kutoa huduma muhimu ya za tiba na upasuaji wa wagonjwa wanaopokelewa na hivyo kupunguza vifo na rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi” alisema Mvungi.
Akizungumzia kuhusu upasuaji wa kitaalamu wa mgongo (specialized Spine Surgeries), alisema taasisi hiyo imeendelea kufanya na zaidi ya asilimia 99 ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wamepona na kurudi katika hali zao za kawaida.
Naye Meneja ustawi wa jamii na uhusiano, Almas Juma, alisema zaidi ya wagonjwa 1,256 wa upasuaji mkubwa wa nyonga walipasuliwa salama na zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa hao wamepona kabisa.
Alisema taasisi imeendelea kutoa matibabu ya maradhi ubongo yaliyokuwa yanahitaji upasuaji yamefanikiwa kufanyika kwa zaidi ya asilimia 80 na wagonjwa waliokuwa na matatizo hayo wamepona na kuondolewa kwenye hatari ya kupoteza uhai.