STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26 Oktoba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa ni wajibu wa wakuu wa mikoa na wilaya kupanga ratiba maalum za kutembelea wananchi mara kwa mara kusikiliza matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi.
Amesema kazi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya si ya kukaa ofisini tu bali ni kazi ya kushughulikia matatizo ya wananchi kwa kuwatembelea kusikiliza shida zao, kusikiliza maoni yao na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akihitimisha mkutano wa siku moja na wakuu wa Mikoa na Wilaya za Unguja na Pemba uliofanyia Ikulu jana, Dk. Shein aliwataka watendaji wakuu hao wa Mikoa na Wilaya kufanyakazi kwa kujiamini na kamwe wasiwakimbie wananchi.
“msikae maofisini, pangeni ratiba maalum… msiwakimbie wananchi, nendeni kwao mkawasikilize na mkabiliane na matatizo waliyonayo”alisisitiza Dk. Shein na kuongeza kuwa wanapokwenda huko hawana budi kujiandaa isiwe ni jambo la kubahatisha.
Aliwaambia kuwa ni wajibu wao kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi na pale ambapo wanakosa majibu ya haraka waahidi kuyatolea majibu wakati mwingine.
Kuhusu migogoro ya ardhi ambayo inaonekana kushamiri hivi sasa, Mhe Rais aliwaeleza watendaji wakuu hao wa Mikoa na Wilaya kuwa wanapaswa kuwa majasiri katika kubaliana nayo na wakati mwingine watalazimika kuchukua maamuzi magumu.
“Jukumu letu ni kushughulikia mogogoro ya ardhi na muhimu zaidi tunapaswa kuzifahamu sheria za ardhi na kuzitekeleza na endapo hatuzifahamu tunapaswa kuwaita wataalamu wa sheria kutoka wizara husika kusaidiana kuitatua” Dk. Shein alisisitiza.
Mhe Rais aliwakumbusha wakuu hao wa Mikoa na wilaya kuwahakikisha watumishi wa ofisi zao wanaelewa vyema majukumu ya Ofisi za Mikoa na Wilaya na hivyo hivyo kwa wananchi wa mikoa na wilaya zao.
Aidha, aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini kwa kuwa uteuzi wao umefanyika kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia sifa na weledi hivyo Serikali imeridhishwa na uwezo wao wa kuzitumikia nyadhifa hizo.
“Serikali inaamini kuwa kwa sifa zenu za utendaji kazi kitimu, kujituma kwenu, kujiheshimu kwenu, uadilifu wenu na sifa nyenginezo mtakidhi matarajio ya serikali na wananchi” Dk. Shein aliwaeleza.
Aliwaambia kuwa kazi yao kubwa ni kubadilii mazingira ya mikoa na wilaya wanazoziongoza na wataweza kufanya hivyo kama wataimarisha mashirikiano na watumishi walio chini yao na wananchi kwa jumla.
Kwa hivyo alihimiza kuweka utaratibu wa vikao vya kawaida vya kila ngazi katika ofisi zao ili masuala mbalimbali yanayohusu ofisi na watumishi yaweze kuzungumzwa na kama ni changamoto ziweze kutafutiwa ufumbuzi kwa pamoja.
Katika mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Joseph Meza, Dk Shein alisisitiza pia umuhimu wa wakuu wa Mikoa na Wilaya kutafuta ushauri au kukubali kushauriwa kwa kuwa hiyo ni njia mojawapo ya kuimarisha uongozi wa pamoja katika sehemu zao za kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi na Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwakumbusha wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia utaratibu uliowekwa na Serikali wa kuwasiliana na wananchi.
“ni lazima tuutumie utaratibu uliowekwa na serikali wa kuwasiliana na wananchi mara kwa mara ili kuwaeleza masuala mbalimbali ya serikali ikiwemo utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo” alisema Dk. Abdulhamid.
Alibainisha kuwa Serikali imekuwa ikitekeleza kwa mafanikio makubwa miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wananchi hawakosa taarifa muhimu za miradi hiyo kutokana na viongozi kutowasiliana nao mara kwa mara.
Katika mnasaba huo, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi aliwataka wakuu hao kutembelea maeneo yao ya kazi kijiji kwa kijiji ili kuyafahamu na pia kupata fursa kukutana na wananchi.
“Ni muhimu uwepo wa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya uonekane katika kila eneo la mkoa na wilaya ili wananchi wamfahamu na waweze kuwasiliana nae” Dk. Abdulhamid alisema.
Aliwaeleza kuwa ni muhimu kwao kujiwekea lengo la kufanya jambo kubwa angalau moja la maendeleo litakalokuwa kumbukumbu nzuri ya uongozi wao na kuwafanya wananchi wawakumbuke watakapomaliza utumishi wao katika mikoa na wilaya walizoziongoza.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822