HOJA YA MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR KULIOMBA BARAZA LA WAWAKILISHI KUTOA MAAZIMIO KUHUSU UIMARISHAJI WA HUDUMA ZA AFYA ZINAZOTOLEWA KWA WANANCHI WA ZANZIBAR.
(Chini ya kanuni ya 27(1) (n), 27(3), 49(1) na 50 ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012)
Octoba, 2014.
HOJA YA MJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR KULIOMBA BARAZA LA WAWAKILISHI KUTOA MAAZIMIO KUHUSU UIMARISHAJI WA HUDUMA ZA AFYA ZINAZOTOLEWA KWA WANANCHI WA ZANZIBAR.
(Chini ya kanuni ya 27(1) (n), 27(3), 49(1) na 50 ya Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012)
MAELEZO YA HOJA.
Kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wake Dr. Ali Mohammed Shein, imekuwa na malengo ya dhati ya kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake, ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kulijenga Taifa lao;
Na kwa kuwa katika kuhakikisha kwamba lengo hilo linatimia, Serikali imekuwa na Sera, Sheria, pamoja na mikakati mizuri ya kuwapatia wananchi huduma bora za afya;
Na kwa kuwa Serikali inaelewa kwamba, maendeleo ya nchi yoyote yanategemea nguvu kazi ya wananchi wake, ambayo inapatikana kutoka kwa wananchi wenye afya iliyo imara;
Na kwa kuwa, Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali za kuimarisha huduma hizo mijini na vijijini, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya afya katika maeneo mbali mbali, ili kuziweka karibu huduma za afya kwa wananchi, lakini pia jitihada za kununua vifaa vya matibabu ili kukabiliana na magonjwa mbali mbali yanayoendelea kuzuka katika jamii yetu siku hadi siku;
Na kwa kuwa, katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa na watu wenye utaalamu wa hali ya juu, Serikali husomesha wataalamu nje ya nchi lakini pia imeanzisha Chuo cha Elimu ya Sayansi ya Afya kilichopo Mbweni, ili kuweza kuwasomesha wananchi wa Zanzibar katika fani mbali mbali zinazohusu maswala ya afya, ili hatimae wataalamu hao waweze kutumika katika hospitali na vituo vya afya vilivyopo nchini kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi;
Na kwa kuwa sisi, viongozi na wawakilishi wa wananchi, tunazishuhudia na kuziona jitihada hizi ambazo zina azma ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na hivyo kupaswa kuziunga mkono;
Na kwa kuwa, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa katika hospitali zetu ni nzuri, bado kuna changamoto kubwa katika kufikia azma hiyo kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu, ukuaji wa teknolojia na kasi ya kuibuka kwa magonjwa mapya;
Na kwa kuwa, tegemeo kubwa la wananchi wa Zanzibar ambao hawana uwezo wa kupata matibabu nje ya nchi, lipo kwa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ambayo Serikali ina lengo la kuifanya kuwa Hospitali ya rufaa, na Hospitali nyengine za Serikali pamoja na vituo vya afya, sisi wawakilishi wa wananchi hatuna budi kuikumbusha Serikali kwamba kuna kazi kubwa ya kuiimarisha Hospitali hiyo kuu kwa Zanzibar na hospitali nyengine ndogo ndogo, Hivyo basi, jitihada za makusudi na za haraka ni lazima zichukuliwe ili kukuza kiwango cha huduma kinachotolewa katika hospitali hiyo, pamoja na kuziimarisha hospitali nyengine ndogo ndogo ili ziweze kutoa huduma za awali kabla tatizo halijapelekwa katika hospitali ya rufaa;
Na kwa kuwa, kwa hali ilivyo sasa, hospitali hiyo ya Mnazimmoja na nyengine nchini zinakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa afya katika fani mbali mbali, ambao wanahitajika kutoa huduma za maradhi makubwa, ambayo yanaonekana kuwakabili wananchi wengi wa Zanzibar;
Na kwa kuwa takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kwamba hali ya upungufu huo wa wataalamu ni kubwa sana. Kwa mfano takwimu zilizotolewa na Mhe Waziri wa Afya wakati akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2012/2013 katika kiambatanisho namba 10, zinaonyesha hali halisi ya mahitaji ya wafanyakazi katika hospitali ya Mnazi Mmoja, Ambapo kwa ujumla zinaonyesha kwamba mahitaji ni makubwa sana kuliko kiwango kilichopo sasa. Kielelezo hicho kinaambatanishwa pamoja na maelezo haya.
Na kwa kuwa upungufu huo wa wataalamu na vifaa unapelekea baadhi ya magonjwa mengi kama maradhi ya moyo, figo, saratani n.k kushindikana kutibika ndani ya nchi, kitendo kinachoilazimisha Serikali kutumia fedha nyingi kuwatibu wananchi nje ya nchi. Takwimu za kibajeti za kila mwaka kwa mujibu wa Hotuba za Bajeti za Wizara ya Afya kwa miaka iliyotajwa, zinaonyesha Kiwango cha fedha zinazotumika kutibu wananchi nje ya nchi kama inavyoonekana hapa chini;
- 2009/2010 –jumla ya dola za kimarekani 369,238 zimetumika kuwatibu watu 73 nje ya nchi.
- 2010/2011 – jumla ya shilingi 906,295,038 zimetumika kuwatibu wananchi zaidi ya 60 nje ya nchi.
- 2011/2012 – jumla ya shilingi 616,091,417 zimetumika kuwatibu wananchi 157 nje ya nchi.
- 2012/2013 – jumla ya shilingi 990,248,168 zimetumika kuwatibu wananchi 144 nje ya nchi.
- 2013/2014 – jumla ya shilingi 2,597,115,697 zimetumika kuwatibu wananchi nje ya Zanzibar.Na kwa kuwa kuwa kwa mujibu wa uchanganuzi huo, inaonekana dhahiri kwamba fedha nyingi zinatumika kwa matibabu nje ya nchi, mbali na gharama nyengine zinazotumika kuwatibu wananchi Tanzania Bara ambapo fedha hizi zingeweza kutumika kuimarisha hospitali zetu kwa kuwapeleka wataalamu kusomea ujuzi wa kutibu maradhi yanayoshindikana hapa nchini kwa sasa na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu ambapo hatua hiyo ingeweza kuipatia nchi madaktari bingwa wengi na kwa muda mfupi zaidi na hatimae wananchi wangeweza kupata matibabu hayo hapa nchini;Na kwa kuwa, bado wagonjwa wanaokosa nafasi ya kutibiwa nje ni wengi kutokana na ukosefu wa fedha, kama ilivyoelezwa na Mhe Waziri wakati akisoma hotuba ya bajeti ya mwaka 2011/2012 ambapo alisema;“Mhe Spika…………..licha ya kuimarika baadhi ya huduma katika hospitali zetu bado wagonjwa wanaoshindikana nchini ni wengi” (uk 43).“Hali ya uchumi wa nchi yetu umewafanya wengi wa wagonjwa kukwama na wengine kupoteza maisha. Wakati nasoma hotuba hii kuna wagonjwa wasiopungua 190 ambao wanasubiri fedha kupelekwa matibabuni nje ya Zanzibar” (uk 43).Na kwa kuwa hali hii inaonyesha kwamba bado mazingira yanayowezesha kupatikana kwa matibabu bora ndani ya nchi yetu na nje ya nchi hayajafikia kiwango kinachotakiwa kunatokana na uhaba wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya hospitali zinazotakiwa kutoa huduma hizo. Kwa mfano, hospitali ya Mnazi Mmoja, ambayo ndio Hospitali kuu kwa Zanzibar, takwimu za miaka mitatu iliyopita zinaonyesha kwamba fedha zinazotengwa na zinazopatikana kwa ajili ya hospitali hii ni kidogo sana, kuweza kutosheleza mahitaji yake, kama inavyoonekana hapa chini;
Mwaka wa fedha | Fedha zilizotengwa | Fedha iliyopatikana kwa mwaka | Asilimia. |
2011/2012 | 262,178,000 | 197,839,870 | 75% |
2012/2013 | 642,000,000 | 410,785,739 | 63% |
2013/2014 | 1,291,199,000 | 664,673,500 | 54% |
2014/2015 | 8,282,000,000 | - | - |
Chanzo: hotuba za Bajeti za Wizara ya Afya kwa miaka iliyotajwa.
Hivyo, kwa takwimu hizi inaonyesha kwamba, kuna haja ya Serikali kuweka kipaumbele cha huduma za afya kwa kuongeza kiwango cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya huduma hizi, ikiwemo vifaa, kusomesha wataalamu, kununua madawa n.k;
Na kwa kuwa, inaonekana kwamba, Serikali inaongeza jitihada ya kusomesha wataalamu wa afya katika fani mbali mbali, ili kuzipa uwezo hospitali zetu kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi, hata hivyo takwimu zinaonyesha kwamba, idadi ya wataalamu wanaopelekwa kusoma ni ndogo na hawajielekezi katika kusomea fani ambazo zina upungufu wa wataalamu nchini; kwa mfano takwimu za wanafunzi waliokwenda masomoni kwa mwaka 2013/2014, zinaonyesha kwamba, jumla yao ni (142), kati ya hao (78) wanasomea Nursing, (13) medical laboratories, (12) AMO (Assistant Medical Officer), (11) ni M.B.B.S, na waliobaki (28) ni katika fani nyengine tofauti. Hivyo, kiwango cha kuwasomesha wataalamu katika fani zinazohusu magonjwa sugu yanayowakabili wananchi ni ndogo, mfano takwimu za mwaka huo huo zinaonyesha kwamba, maeneo muhimu kama ya ENDOCRINOLOGY (yanayohusu magonjwa ya sukari), ORTHOPEDIC SURGERY (yanayohusu tiba ya wagonjwa waliovunjika viungo), ONCOLOGY (yanayohusu matibabu ya cancer) na PEDIATRICIAN (yanayohusu tiba za watoto wadogo), INTERNAL MEDICINE (yanayohusu tiba ya maradhi ya moyo, mapafu n.k), na maeneo mengineyo, wataalamu waliokwenda masomoni ni mmoja mmoja tu kwa kila fani. (takwimu hizi kwa mujibu wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2014/2015 uk 83).
Na kwa kuwa, takwimu za wataalamu wanaorudi masomoni wengi ni wa ngazi ya chini kuliko ngazi ya juu, hali inayopelekea kukosa wataalamu mabingwa wa kutibu maradhi mbali mbali, kwa mfano takwimu za wanafunzi waliorudi masomoni kwa mwaka 2012/2013, wengi ni katika ngazi ya cheti (14) na ngazi ya degree ya kwanza (38), kati ya hao (16) wanasomea Nursing, katika ngazi ya post graduate ni (1), ngazi ya masters ni (4) na ngazi ya PHd ni (1). (Takwimu hizi kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2013/2014 uk 101).
Hii ni dhahiri kwamba, bado kuna kazi kubwa ya kujielekeza katika kuwekeza katika kusomesha wataalamu wengi, ili kuweza kuepuka matumizi ya gharama kubwa za kuwatibu wananchi nje ya nchi, lakini pia kuwapatia wananchi huduma bora zaidi za afya.
Na kwa kuwa, Ili kuhakikisha kwamba hatua za haraka zinachukuliwa na Serikali ili kuweza kuondoa mapungufu hayo na kuhakikisha kwamba huduma za kuridhisha zinapatikana katika hospitali zetu,
Na kwa kuwa sisi wawakilishi wa wananchi tuna jukumu la kuisimamia Serikali katika kuhakikisha kwamba majukumu yake yanatekelezwa katika kiwango cha kuridhisha, kwa kuishauri Serikali katika mambo mbali mbali yanayohusu maslahi ya wananchi likiwemo suala hili muhimu la afya;
Hivyo basi, mimi Jaku Hashim Ayoub, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia jimbo la Muyuni, chini ya Kanuni ya 27(1) (n), 27(3), 49(1) na 50 ya kanuni za Baraza la Wawakilishi toleo la 2012, naliomba Baraza lako tukufu lipitishe maazimio yafuatayo:-
- Kwamba Serikali ifanye mabadiliko ya kisera yatakayoiwezesha Serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuwasomesha wataalamu wetu nje ya nchi, ili waweze kuwahudumia wananchi badala ya kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kupeleka wagonjwa nje ya Zanzibar;
- Kwamba, mabadiliko hayo ya kisera yaende sambamba na kuwa na mkakati wa kusomesha kwa awamu wataalamu wa fani ambazo zina upungufu, hususan katika magonjwa sugu yanayoshindikana kutibiwa ndani ya Zanzibar, na kuacha kujikita katika kusomesha wataalamu katika fani hizo kwa hizo, ambazo tayari zina wataalamu wa kutosha;
- Kwamba Serikali ifanye mabadiliko ya kimfumo wa kibajeti, kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016, utakaowezesha kupunguza kwa kiwango maalum bajeti zinazotengwa katika sekta nyengine, ili kuweza kuongeza kiwango cha bajeti inayotengwa kwa ajili ya sekta ya afya nchini, itakayowezesha ununuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu pamoja na kusomesha wataalamu mabingwa wa maradhi mbali mbali;
- Kwamba, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ihakikishe kwamba fedha zinazotengwa katika Bajeti ya Serikali kwa ajili ya kugharamia huduma za afya zinaingizwa zote na kwa wakati, ili Wizara ya Afya Iweze kutimiza wajibu wake kama inavyojipangia;
- Kwamba, Serikali ifanye mabadiliko ya mishahara na maslahi ya wataalamu wa afya, ili kuwapa moyo wataalamu wetu na hivyo waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, lakini pia kuwa na maslahi mazuri yatakayopelekea wataalamu hao kubaki nchini na kuwahudumia wananchi.
- Kwamba, Wizara ya Elimu na Bodi ya Mikopo Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, wajielekeze katika mpango wa muda mrefu wa kusomesha na kupata wataalamu mabingwa wa maradhi mbali mbali hapa nchini.
- Kwamba, Serikali iandae mkakati madhubuti na wenye kutekelezeka ndani ya muda mfupi, kwa ajili ya kujaribu kuwarejesha nchini wataalamu mabingwa wa maradhi mbali mbali waliokimbilia sehemu mbali mbali duniani kwa sababu mbali mbali ikiwemo maslahi.……………….Jaku Hashim Ayoub,Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (jimbo la Muyuni),Zanzibar.