Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein: Zanzibar inajivunia ushirikiano wake na UN pamoja na mashirika yake

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                                             27 Oktoba, 2014


TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inajivunia ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa na Mashirika yake  kwa kuwa ushirikiano huo umekuwa wa manufaa kwa pande zote.
Amesema Zanzibar inaridhishwa na ushirikiano huo na kuupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuanzisha ofisi za baadhi ya mashirika yake kisiwani Unguja jambo ambalo limezidi kuimarisha ushirikiano huo kwa kuwa limeuweka umoja huo karibu na wananchi wa Zanzibar.  
     

Akizungumza na Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bwana Alvaro Rodrigez Ikulu leo, Dk. Shein alimueleza Bwana Rodrigez kuwa chini ya ushirikiano huo Zanzibar imeweza kushirikiana na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alibainisha kuwa misaada inayotolewa na Umoja wa Mataifa kupitia mashirika na taasisi zake imekuwa chachu na kuongeza kasi ya jitihada za Serikali na wananchi katika utekelezaji wa malengo ya mipango ya maendeleo na pia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Dk. Shein alitoa mfano wa mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango wa kijiji cha mfano cha Milenia cha Kiuyu Mbuyuni huko katika wilaya ya Micheweni ambao unaangalia utekelezaji wa malengo ya Milenia kuwa umebadili kabisa maisha ya watu wa kijiji hicho.



Aidha, alisema kupitia mradi wa redio jamii, unaoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na UNESCO wananchi wameweza kuelimishwa masuala mbali mbali ya maendeleo na kijamii na pia wameweza kuitumia redio hiyo kuzungumza na kujadili masuala hayo kwa uwazi.

Matokeo yake, alimueleza bwana Rodrigez, mtazamo wa maisha wa wananchi wa huko umebadilika na hivi sasa watoto wote wanakweda skuli, wananchi wanatumia huduma za afya pamoja na kujenga nyumba za bora.

Kwa hivyo alieleza mafanikio hayo ni miongoni mwa mifano mingi ya namna Umoja wa Mataifa na Mashirika yake yanavyoshiriki katika kuleta mabadiliko ya maisha ya kila siku ya wananchi ulimwenguni ikiwemo Zanzibar.

Kuhusu utekelezaji wa malengo ya Mipango mbalimbali ya Maendeleo, Dk. Shein alieleza kuwa pamoja na Zanzibar kuweza kufikia baadhi ya malengo ya Milenia kama vile uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda skuli, lakini inakabiliwa na changamoto nyingi.

Alibainisha kuwa lengo kuu la Dira ya mwaka 2020 ya kuifanya Zanzibar kuwa nchi yenye uchumi wa kati linaendelea kutekelezwa kwa bidii na matumaini ya kufikiwa yapo lakini ikiwa imebaki miaka mitano ni lazima kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili nchi hivi sasa.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana, kukosa wa maarifa na ujuzi kwa wajasiriamali pamoja na uhaba wa mitaji.

Changamoto nyingine alizitaja kuwa ni tatizo la kuongezeka kwa kasi ya uhamiaji mijini na mwelekeo mpya wa watu kuhama mijini na kuvamia maeneo yaliyo karibu na miji yasiyopimwa na msongomano wa wanafunzi madarasani.

Kwa hivyo alimueleza Mratibu Mkaazi huyo wa Umoja wa Mataifa kuwa Zanzibar ingependa kuona umoja huo kupitia mashirika yake unashirikiana zaidi na Zanzibar kukabiliana na changamoto hizo ili kufanikisha malengo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii yaliyowekwa na  Serikali.

Dk. Shein alisisisitza kuwa ni muhimu kuendelea kufanya kazi pamoja unatokana na ukweli kuwa pamoja na changamoto hizo Zanzibar bado inakabiliwa na tatizo la rasilimali ikiwemo fedha na watumishi wenye ujuzi hivyo inahitaji kujengewa uwezo ili iweze kutekeleza mipango yake kwa ufanisi na kutoa matokeo yanayotarajiwa.

Kwa upande wake Bwana Rodrigez alimpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake bora katika kuiongoza Serikali ya Mapinduzi iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Alisema katika kipindi cha uongozi wake hadi sasa Serikali imeweza kushirikiana vyema katika kutekeleza miradi mbalimbali kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake na kupongeza hatua ya Serikali kupitisha sheria kuhusu Ugonjwa wa UKIMWI na pia Sheria ya Kuanzisha Baraza la Baraza la Vijana Zanzibar.

Bwana Rodrigez alieleza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha mipango yake ya uchumi na maendeleo ikiwemo MKUZA II pamoja na Mpango wake Uchumi wa Miaka Mitano.

Alieleza kuwa dhamira ya Umoja wa Mataifa hivi sasa ni kujenga mfumo wa uendeshaji na utekelezaji miradi ambao utakuwa na manufaa katika nyanja zote ya maisha zote maisha ya watu katika eneo la mradi.

 



Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 


                                               

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>