Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Rwanda Balozi Said Ali Siwa akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Barala la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Rwanda Bwana Said Ali Siwa aliyefika Ofini kwake Baraza la Wawakilishi kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo(Picha na OMPR.)
Na Othman Khamis OMPR.
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rwanda zina wajibu wa kuendelea kushirikiana pamoja katika kudumisha udugu na ujirani mwema kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Rwanda Balozi Said Ali Siwa aliyekuja kuaga rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo katika jengo la Baraza la Wawakilishi liliopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif Alisema Rwanda na Tanzania zimekuwa na mafungamano ya karibu kwa muda mrefu hasa ule wakati wa Mataifa hayo yakipigania kupata uhuru kutoka kwa wakoloni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi Said Ali Siwa kuhakikisha kwamba anasimamia vyema uhusiano huo ambao unaonekana kupata majaribu wakati Rwanda ilipokuwa na sintofahamu wa vurugu za Kisiasa zilizosababisha vite vya Kikabila Nchini humo.
Alisema Tanzania ililazimika kipindi hicho kupokea wakimbizi wa Rwanda ambao walihitaji kupata hifadhi kutokana na vurugu hizo zilizoleta maafa makubwa Nchini Rwanda.
Hata hivyo Balozi Seif alimtahadharisha Balozi Said kuwa tayari kupambana na changamoto atazokabliana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya Kidiplomasia Nchini Rwanda.
Balozi Seif aliipongeza Serikali ya Rwanda kwa jitihada ilizochukuwa za kurejesha hali ya utulivu miongoni mwa wananchi wake .
Mapema Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Rwanda Bwana Said Ali Siwa alisema uteuzi alioupata ni fursa kubwa na ni muhimu kwake katika muelekeo wa kutekeleza jukumu alilokabidhiwa na Taifa.
Balozi Said alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba atakuwa tayari kuchota fikra na mawazo ya waliomtangulia ili kuona kazi yake ya Kidiplomasia inakwenda katika matarajio yaliyokusudiwa.
Alisema muda wote hatosita kuchota uzoefu alionao Balozi Seif kwa lengo la kutekeleza vyema na makini majukumu aliyopangiwa.