Na Salim Said Salim
UAMUZI wa Vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu mwakani umeelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva kuwa halali na hauna dosari ya kisheria. Vyama vinavyounda huu ni NCCR-Mageuzi, CUF, CHADEMA na NLD.
Si ajabu tukasikia katika siku chache zijazo kauli aliyotoa Jaji Lubuva Dodoma karibuni aliposhiriki katika semina ya Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania ya kuhamasisha wadau wa siasa kudumisha amani, ikazusha jambo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM.
Tusibiri na tutaona namna viongozi hawa wanaotaka sheria zitafsiriwe wanavyotaka wao tukawasikia wanasema “haiwezekani” na kuanza kujenga mizengwe ya kutaka Ukawa wazuiliwe kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu umoja wao kwa kiasi fulani unaweza kuidhoofisha CCM katika huo uchaguzi.
Sitashangaaa tukiona kuwepo kwa wanasheria ambao walikuwa wakiheshimika sana nchini siku za nyuma, hasa juu ya masuala ya katiba wakatumukia kuutia mueleka msimamo kwa kuupa sura ya kukiuka sheria za nchi na ya vyama vya siasa.
Kwa jinsi wanasheria hawa walivyobadilika siku hizi na kushangaza watu wengi, wakiwemo wanafunzi wao, sitaona ajabu nikiwasikia wakija na mpya ya kusema kutoipa kura CCM ni kuvunja katiba na kutomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Watu hawa wananaweza kufaya hivi kwa sababu wameonesha hivi karibuni dalilili za kufilisika katika taaluma ya sheria. Ni kawaida mtu anayefilisika kifedha au kitaaluma au hata kiakili kufanya mambo ya ajabu ajabu ambayo huwa hayategemewi.
Kwa watu wanaofilisika, kwa njia moja au nyingine, kwao pochi hua ndio muamuzi wa mwelekeo wao na sio jingine. Watu hawa husahau hata kauli na maandishi yao ya siku ziliopita ambayo yaliwajengea heshima ndani na nje ya nchi.
Kwa baadhi ya viongozi wa CCM wanaojifanya wanajua sana historia ya nchi hii na kwamba wao ndio wenye uchungu mkubwa na Muungano kuliko watu wengine wanaweza kuja na maelezo ya kututaka tuone kwa kauli ya Jaji Lubuva imelenga “kuhatarisha amani na utuliu”.
Hata vyombo vya habari hapa nchini ambavyo baadhi ya waandishi wake waandamizi wamekuwa wakibebeshwa mizigo ya kupaka matope vyama vingine na wagombea wao tutawaona wanabeba bango la kupinga uamuzi wa Ukawa.
Katika karibu chaguzi zote zilizopita tulishuhudia kuwepo waandishi wa habari, wakiwemo wale wanaoitwa waandamizi, waliojifanya wapagazi wa mizigo ya siasa za fina, chuki na ubaguzi.
Namna ambavyo waandishi wachache walivyojizatiti kuudanganya umma ili kumchafulia jina mwana diplomasia maarufu Waziri Mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim, ni kigezo tosha cha namna wanasiasa wanavyotumia vyombo vya habari kufikia malengo yao machafu.
Waandishi wa habari wengine walikuwa ni kama mameneja wadogo wa wagombea na hata kubeba kikapu cha fedha kulipa waandishi wanaofuatilia mikutano ya kampeni ya wagombea wanaowapigia debe.
Zipo taarifa ambazo ukweli wake wanajua wahusika walishukuriwa kwa mchango wao kwa kupewa nyadhifa mbali mbali serikalini na sasa ni wanasiasa na taaluma ya habari imekuwa sehemu ya historia ya maisha yao.
Hali kama hiyo ya kuchafuliana majina au kutengeneza mazingira kukikwamisha chama au mgomea katika uchaguzi ni kawaida kuona inafanyika wakati wa uchaguzi kwa wale wawanoona matumizi ya njia chafu ni siasa safi.
Hii ni kwa sababu ni kawaida kwa mtu anayefanya maovu kumtilia shaka kila mtu anayeona kauli au kitendo chake hakimfurahishi.
Sitaona jambo la ajabu kama Jaji Lubuva ambaye hana historia ya kujihusisha na siasa akapitwa “sio mwenzetu”, kama walivyofanyiwa majaji wengi mashuhuri wa nchi hii.
Orodha ya majaji waliovunjiwa heshima yao na kazi yao iliyotukuka kuonekana ni ya kipuuzi chini chini na hadharani ni ndefu mongoni. Miongoni mwao ni aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali, Jaji Robert Kissanga na hivi karibuni Jaji Warioba.
Tatizo waliokuwa nalo hawa wanaojiita wakereketwa wa CCM ni kuangalia wanasheria na hasa majaji kwa mitazamo ya kisiasa na sio kwa misingi na maadili ya taaluma ya sheria.
Jaji Lubuva alisema viongozi wa Ukawa wanaposema katika wilaya fulani watasimamisha mgombea wa mmoja, hawaundi chama na sheria inaruhusu.
Tayari tumeshaona viongozi wa badhi ya vyama vya upinzani vimeshaanza kupiga kengele inayoashiria kutofurahishwa na uamuzi wa Ukawa. Kinachosubiriwa ni kumpata panya atayeweza kumfunga paka hiyo kengele.
Watanzania tumekuwa tukiambiwa kuwa umoja ni nguvu.
Lakini kwa hili la vyama vilivyounda Ukawa la kutangaza nia yao ya kutaka kuunganisha nguvu zao katika uchaguzi ujao si ajabu tukaja tukaambiwa uamuzi wao kuunganisha nguvu zao linataka kudhoofisha amani ya nchi na kuipeleka nchi yetu pabaya.
Suala hili kama litawekewa vizingiti kwa kutafuta vsingizio vya kisheria kama halijachukuliwa tahadhari linaweza kuzusha mvutano mwingine wa kisiasa nchini na hata kuathiri uchaguzi wa mwaka 2015.
Ni vizuri kuziachia sheria za nchi yetu na demokrasia kufuata mkondo wake badala ya kutaka utashi wa kisiasa kuamua sheria za nchi yetu ziwe na mwelekeo gani.
Wakati kama huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu hali ni tete na lazima kwanza tuhakikishe tunaziheshimu sheria na hatutafuti njia za kuzipinda ili kukidhi utashi wetu wa kisiasa kwa lengo la kutupatia ushindi.
Ni vyema hekima na busara zikatumika ili huu uamuzi wa
Ukawa usitupeleke pahala pabaya na kuwa chanzo cha kuwasha moto ambao hatuna uwezo wa kuuzima.
Lakini kwa upande mwingine vyama vinavyounda Ukawa vinapaswa kuelewa kuwa suala hili ni gumu na zito na kwamba miongoni mwao wataweka maslahi yao binafsi na sio vya vyama vyao na nchi na wanaweza hata kuzusha mivutano na vurugu katika uamuzi huu kama hawatachaguliwa kuwa wagombea.
Tumewaona baadhi ya wana siasa katika CCM, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na vyama vingine kuacha vyama pale wanapokosa kura za maoni na kuhamia vyama vyengine dakika za mwisho ili wawe wagombea.
Hapa panaweza kuzuka mizengwe ya kila aina mbali na wakati wa kutafuta wagombea inayohusu hivyo vyama vinavyounda Ukawa moja kwa moja. Mizengwe hii inaweza kuwa na uhusiano na mambo ambayo ni nyeti sana kama ya dini na kabila.
Ni vizuri kuweka maslahi ya nchi mbele kuliko ushindi katika uchaguzi. Kama hatujachukua tahadhari mapema tunaweza kujijutia kwa kuweka mizengwe ya siasa chafu au ubinafsi mbele katika uchaguzi ujao.
Chanzo : Tanzania Daima