Na Shehe Semtawa
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeanzisha mikakati mbalimbali ambayo lengo lake ni kuvutia wawekezaji ambao watasaidia wananchi katika kuwakomboa kiuchumi na kukuza biashara zao.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuweka milango wazi kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambao ni muhimu katika nchi zinazoendelea.
Hata hivyo, serikali inaamini kuwa ushirikiano kati yake na Kituo cha Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), na taasisi nyingine utasaidia kuboresha uchumi wake.
Pia inahakikisha Zanzibar inajiendeleza katika uzalishaji wa bidhaa bora na hatimaye kuwa kivutio kikubwa cha bidhaa bora na nchi jirani.
Moja ya mfano mzuri ni kampuni inayojishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa ya nyama bora ya kuku (Zanchick), ambayo ilianza mradi wa uwekezaji katika Zanzibar mwaka 2011.
Kampuni hiyo inaingiza mapande ya nyama ya kuku kutoka Marekani kwa kila mwezi makontena saba.
Kuanzishwa mradi huo kumeleta matokeo chanya ambapo umewafanya Wazanzibari wengi kufaidika kutokana na shughuli moja au nyingine zinahusiana biashara hiyo ya uuzaji wa nyama ya kuku.
Akifafanua zaidi juu ya umuhimu wa uwekezaji katika kisiwa hicho, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Issa Kassim (Baharia), anasema uwekezaji wake utakuwa na uwezo wa kufikisha malengo ya uwekezaji ikiwemo kukuza soko la ajira na ukuaji wa uchumi.
Katika kukuza soko la ajira na mapambano dhidi ya umaskini, kampuni hiyo hadi sasa tayari imetoa ajira za moja kwa moja kwa vijana zaidi ya 300 wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi katika kiwanda na mtandao wa usambazaji, ambao ni pamoja na maeneo ya Unguja na Pemba.
“Lengo la kampuni hii ni kuinua sekta ya uwekezaji na kuhakikisha kila raia anapata ajira, hatua ambayo anaamini itahamasisha ukuaji wa biashara ya mtu binafsi.
"Zanchick ni mkombozi kwa sababu sasa imeleta ushindani wa bei, hivyo nyama hiyo ya kuku kupatikana kila mahali tena kwa urahisi hivyo kufanya kila mtu sasa anaweza kula kuku,” anasema Baharia.
Baharia anasema kampuni hiyo haiuzi bidhaa zake kwa bei ya rejareja, bali inauza kwa bei ya jumla ambako wajeja wake wakubwa ni hoteli, migahawa na mawakala wanaume na wanawake ambao wanafanya biashara hiyo, ya usambazaji huku wakinufaka kwa kujipatia faida ambayo huwasidia kutanua biashara zao.
Anasema kampuni ina miaka mitatu tangu kuanza shughuli zake, na tayari imejenga kiwanda cha usindikaji wa nyama hiyo kuku iliyotiwa viongo ikiwa ni kuongeza thamani na ubora wa bidhaa hiyo.
“Kampuni pia hununua kiasi kikubwa cha viungo mitaani kwa ajili ya kituo uzalishaji ikiwa ni hatua za kuongeza radha katika bidhaa yake ya nyama ya kuku,” anasema Baharia.
Mipango ya baadaye
Kampuni hiyo ina mipango ya kujenga kituo kikubwa ambacho kitakuwa kikizalisha bidhaa mbalimbali katika sekta hiyo, na kwamba pia kitakuwa na uwezo wa kuongeza thamani bidhaa zake, ili ziweze kuwa na viwango vinavyohitajika katika soko.
“Hivi sasa lipo jengo jipya kwa ajili ya uzalishaji ambalo iliyojengwa katika kipindi cha Julai ya mwaka huu, ambapo awali tulianza na ofisi moja, hii ni hatua ya kwanza katika kufanya Zanzibar kikanda kuwa na wasambazaji wenye uwezo wa kuongeza thamani bidhaa ya kuku.
“Lakini kama hiyo haitoshi pia hivi sasa, tuko katika mazungumzo na mashirika yasiyo ya kiserikali na vyanzo vingine, ili kuanzisha uhusiano utakaosaidia kuzalisha na kusambaza nyama ya kuku wanaozalishwa hapa hapa Zanzibar.
“Lengo ni kuunga mkono jitihada za Wizara ya Mifugo Zanzibar, ambapo kampuni itaratibu mipango ya kusaidia wakulima wa ndani, kwa kutoa chanjo na elimu juu ya teknolojia ya kisasa na mambo muhimu ya ufanisi katika masuala mabalimbali ya ufugaji," anasema Baharia.
Meneja Uendeshaji, Andre De Lange, anasema kampuni ina mipango siku za usoni kutoa fursa kwa wafugaji wa Zanzibar kuuza kuku wao katika kampuni hiyo, hayo yatafanyika baada ya wafugaji kupatiwa mafunzo ya ufugaji bora na wakisasa zaidi.
Mfanyabiashara atoa ushuhuda
Mfanyabiashara Rashid Mohammed, anasema yeye ni miongoni mwa watu waliokombolewa na Zanchick.
Anasema awali alikuwa akiuuzwa mishikaki, alikuwa na wakati mgumu wa kupata kuku na hata akiwapata walikuwa ni kwa bei ya juu.
Mohammed, anasema siku moja kupitia televisheni aliona tangazo la kampuni ya Zanchick, likitangza ubora wa bidhaa zake huku zikiwa na bei nafuu na siku iliyofuata alikwenda kununua kuku.
“Nakumbuka siku hiyo baada ya kununua ndani ya saa 48, nipata faida ya sh 30,000, nikagundua kuwa sasa nimepata mgodi wa dhahabu unaotembea,” anasema Mohammed.
Anasema bidhaa za Zanchick ni salama na zimethibitishwa kuwa zina ubora kwa walaji wa kisiwa hicho ambao asilimia 99 ni waislamu.
“Zanchick imenisaidia sana katika kupanua biashara yangu kwa sababu baada ya kuanza na boksi moja hivi sasa nina uwezo wa kununua maboksi 45 hadi 50 kwa siku, na kuyauza yote,"anasema Mohammed.
Anasema hivi sasa ana maduka matano ya kuuza nyama huku akifanikiwa kutoa ajira kwa vijana wa jinsia zote 12.
“Kutokana na kupanuka kwa biashara yangu hivi nimekuwa maarufu hadi kupewa jina la utani mitaani la ‘Rashid muuza kuku,” anasema Mohammed.
Anabainisha kuwa biashara hiyo imemuwezesha kulipa kodi ya nyumba nzima akilinganisha na mwaka 2011 ambako aliishi katika chumba kimoja ambacho hakikuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya familia yake, na kwamba hivi sasa anajenga nyumba yake ya kisasa.
Mohammed anasema anatarajia kuwapatia elimu bora watoto wake watatu ikichangiwa na mafanikio yaliyotokana na biashara yake hiyo.
Chanzo : Tanzania Daima