Na Hafsa Golo
Msikiti mkubwa unaojengwa na Mfalme Qaboos wa Oman ambao una uwezo wa kusaliwa na waumini zaidi ya 1,000 kwa wakati mmoja, umefikia hatua nzuri ya ujenzi wake na na unatarajiwa kukamilika mwaka 2016.
Hayo yamebainika wakati Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Ali Juma Shamuhuna, alipotembelea msikiti huo kuangalia ujenzi unavyoendelea.
Meneja wa mradi wa ujenzi wa msikiti huo, Mhandisi, Ahmed Khalfan Al-shukaili, alisema ujenzi ulitarajiwa kukamilika mwaka ujao lakini haitowezekana kwa sababu ya kuchelewa baadhi ya vifaa.
Aidha alisema msikiti huo unajengwa kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha unadumu kwa zaidi ya karne moja bila kujitokeza athari.
“Msikiti tunaojenga utapendeza kama Mfame alivyoagiza na Mwenyezi Mungu akijaalia utadumu milele bila kujotokeza hitilafu,” alisema.
Naye Waziri Shamuhuna, alisema msikiti huo pia utakuwa na chuo cha kiislamu kitakaochukua zaidi ya wanafunzi 100 kwa wakati mmoja.
Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Mazizini, Dk. Muhyddin Ahmad (Maalim Siasa), alisema iwapo chuo hicho kitaanzishwa wanafunzi watafundishwa na walimu wazalendo.
Alisema wapo walimu wanne wenye shahada ya uzamivu (Phd) na 21 shahada ya uzamili na kwamba walimu 18 wako masomoni nje ya nchi wakisomesha shahada ya uzamili na uzamivu.