Na Mwandishi Maalum, New York
Nchi zinazoendelea hususani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeshauriwa kujiwekea mipango, sera, taratibu na sheria zinazotekelezeka ambazo kwayo zitaongeza na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili si tu kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wake lakini pia kuwa na maendeleo endelevu.
Aidha nchi hizi zimeambiwa kuwa kile kipindi cha kusubiri kuletewa maendeleo kwa maana ya kuwategemea wafadhili kupitia uwekezaji wa moja kwa moja ( FDI) au misaada kimeshapita kwa kuwa hakuna nchi inayoweza kuleta maendeleo kwa nchi nyingine.
Hayo yamejitokeza siku ya Jumanne hapa Umoja wa Mataifa, wakati wa majadiliano yasiyo rasmi ya mada iliyohusu mapato ya ndani ( public financing) kama njia moja wapo ya uwezeshaji wa maendeleo endelevu. Majadiliano haya yanafanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Tatu wa Kimataifa juu ya Uwezeshaji wa Raslimali Fedha kwa Maendeleo Endelevu. Mkutano utakofanyika mapema mwakani huko Addis Ababa, Ethiopia.
Ujumbe wa Tanzania katika majadiliano haya unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bibi Dorothy Mwanyika.
Mchokoza mada wa majadaliano hayo, Profesa Atul Kohli kutoka Chuo Kikuu cha Princeton cha Marekani, ameeleza si tu kwamba hakuna nchi au mtu anayeweza kumletea maendeleo mwingine lakini pia hakuna mfumo mmoja wa maendeleo ambao unaweza kutumika kwa nchi zote.
Amesema nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zimendelea kuwa nyuma kimaendeleo tofauti na baadhi ya nchi za Asia, kwakuwa zimeendelea kuwa tegemezi wa misaada ya nje na vile vile kuwa na madeni makubwa.
Profesa Kohli amesema, nchi masikini zinaweza kujifunza mambo mawili au matatu kutoka nchi zenye uchumi wa kati kama vile Korea ya Kusini na Malaysia ambazo pamoja na kuwa na utashi wa kisiasa wa kuondokana na utegemezi pia ziliamua kwa dhati pamoja na mambo mengine kuibua vyanzo vya mapato yao ya ndani na kuwa na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato hayo pamoja na matumizi yake.
Aidha amesema hakuna nchi ambayo imeweza kupiga hatua kubwa ya kiuchumi na kimaendeleo pasipo kufanya mageuzi ya viwanda ikiwa ni pamoja na kuvilinda viwanda vyake.
“Hakuna nchi ambayo imeweza kupata mafanikio makubwa katika eneo la viwanda bila serikali kuingilia kati au kusaidia. Ipo mifano hai ya namna ambavyo hata serikali za mataifa makubwa zilifanya katika karne za 18, 19 na 20 kulinda viwanda vyao dhidi ya bidhaa kutoka nje”. Amesema Profesa Atul Kohli.
Uzalishaji wa bidhaa kwaajili ya masoko ya nje ni moja ya eneo ambalo siyo tu linaongeza mapato ya ndani lakini pia inaifanya nchi kutokuwa mwagizaji zaidi wa biadhaa kutoka nje.
Aidha ameeleza kuwa utashi wa kisiasa, nchi imara, viongozi wanaowajibika wasiokuwa waoga katika kusimamia vipaumbele wanavyovipanga ni moja ya sababu ambayo baadhi ya nchi zenye uchumi wa kati zimefika hapo zilipo.
Amesisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na upanuzi wa wigo wa mapato hayo, unahitaji pia watendaji wanaowajibika na ambao wako tayari kuziba mianya ya ukwepaji kodi na wanaowajibika kwa wananchi wao kwa kuwa wanamkataba nao.
“Ni lazima msimamie maendeleo yenu kutokana kile mlichonacho bila ya kutegemea misaada kutoka nje. Imarisheni vyanzo vyenu vya mapato,uwekezaji wa ndani na mitaji ya kijamii. Mnaweza kutegemea misaada ya nje muhimu lazima muwe na mapato yenu imara ambayo hayatawafanya muwe tegemezi”, amesisitiza Profesa Kohli.
Akichangia majadiliano hayo, Naibu Katibu Mkuu, Bibi Dorothy Mwanyika amesema, nchi nyingi zinazoendelea Tanzania uzoefu umeonyesha kuwa upatikanaji wa misaada kutoka nje na inayotolewa kwa wakati na inayotabilika imeweza kutoa unafuu kwa nchi zinazoendelea ambazo hazina uwezo wa kukusanya mapato yake zenyewe.
Hata hivyo ameeleza kuwa hivi sasa nchi zinazoendelea zimegudua kuwa siyo tu kuwa misaada hiyo haitoshi lakini wakati mwigine haitabiriki huku ikiwa ni ya muda mfupi. Na kubwa zaidi sehemu kubwa ya misaada hiyo ikirudi kule ilikotoka ili hali walengwa wakinufaika kidogo.
Akasema ni kutoka na uzeofu huo ndiyo maana Tanzania inathamini mfumo huu mpya wa kuwa na vyanzo tofauti vya mapato vitakavyosaidia kusukuma mbele ajenda za maendeleo endelevu baada ya 2015.
Naibu Katibu Mkuu amesema ni kwa kulitambua hilo ndiyo maana Tanzania imejiwekea taratibu za kuhamasisha raslimali za ndani ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa vyanzo vya mapato yake ukusanyaji wa kodi na kuziba mianya ya ukwepaji kodi pamoja na kupunguza misamaha ya kodi.
Vile vile Bibi Mwanyika amesema, nchi zilizoendelea zinatakiwa kuongeza kasi ya ushirikiano wake katika udhibiti wa utoroshaji wa fedha pamoja na fedha chafu jambo ambao amelieleza kuwa linachangia katika kuzifanya nchi zinazoendelea kukosa mapato ya kutekeleza mipango ya maendeleo.
Naibu Katibu Mkuu pia amegusia suala la mzigo wa madeni kwa nchi zinazoendelea na kueleza kuwa ni mzigo unaozielemea nchi hizo na hasa ikizingatiwa zina lazimika kukopa ili kuziba pengo la upugufu wa mapato yake.