Na Salim Said Salim
WAZIRI Kiongozi mstaafu wa Awamu ya Sita ya Serikali ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, amesema ipo haja ya kuendelea kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Visiwani, kwa vile sababu zilizofanya kuundwa kwake zipo.
Nahodha aliyekuwa akitoa maoni yake wakati serikali hio shirikishi iliyoundwa na CCM na CUF ikiwa imetimza miaka minne wiki iliopita amesema kuundwa kwa SUK kumeisaida Zanzibar kuwa sio tu kuwa na hali ya utulivu wa kisiasa bali pia kupata maendeleo.
Alisema ni vyema watu wa Zanzibar wakafanya tathmini ya manufaa ya mfumo huo wa serikali shirikishi na waangalie faida zake kwa serikali yenyewe na kwa wananchi.
Nahodha alieleza haja ya kutambua kwamba popote pale penye ushindani wa nguvu wa vyama vya kisiasa ni vizuri kwa viongozi wake kugawana madaraka.
Kufumbia macho ukweli huu panaweza kuwa sababu ya kukosekana utulivu ambao ni muhimu katika kuisaidia nchi kupata maendeleo.
Kauli hii ya Nahodha ni ishara ya kwa kiasi fulani kiongozi huyu kukomaa kisiasa, kuukubali ukweli na kuweka uzalendo na maslahi ya Zanzibar mbele badala ya utashi wa kisiasa kwa kutumia visingizio vya historia au kubuni hadithi zenye lengo la kuuhadaa umma.
Lakini ni vizuri wakati huo huo Nahodha akaelewa kuwa kauli yake hii haitawafurahisha wahafidhina na wale ambao hawana uchungu na Zanzibar.
Si ajabu hawa wahafidhina wakaanza kumchimba na kumueleza kuwa “sio mwenzetu” au kumpikia majungu ya kurubuniwa na hata kutafuta mgombea mwengine wa CCM katika jimbo lake la uchaguzi.
Hali kama hii tumeona kuwafika viongozi kadha maarufu wa Serikali ya Zanzibar na CCM, wakiwemo waasisi wa Mapinduzi, kama Mzee Hassan Nassor Moyo na wengine wengi.
Hawa wahafidhina ambao huumia na kukosa raha wakiona Zanzibar imetulia siku zote wamekuwa wakipenda kuendeleza siasa za fitna na malumbano Visiwani.
Lakini ukichunguza utaona wengi wao ambao wasiowapenda wanawaita makenge ni watu wa kufikia na hawana uchungu na visiwa hivi. Huu ndio ukweli na wanaonuna haya yakielezwa shauri yao kwani wangekuwa kweli ni watu wanaoitakia mema Zanzibar wasingekuwa siku zote wamejikita katika siasa za fitna na malumbano yanayoandamana na kauli za kashfa na matusi.
Baadhi ya watu hawa wanatumia muda mrefu Bara na kuja Zanzibar baada ya muda ili kuomba kura katika majimbo yao ya uchaguzi au kupandikiza mbegu za siasa za chuki na wakishafanya hivyo wanarudi Bara haraka.
Hawa ndio wale ambao wahenga walisema ni watu wanaopenda kukaanga mbuyu na kuachia wengine (wakiwemo vibogoyo) kutafuna.
Watu wa aina hii inafaa kuangaliwa kwa uangalifu mkubwa na Watanzania kwa vile wamedhihirisha kuwa ni wabaguzi waliokubuhu. Miongoni mwao ni wale wa kundi la wahafidhina waliofilisika kifedha na kisiasa ambao siku hizi wanatapatapa kama samaki aliyebanwa na ndoana na kutaka watu wa kisiwa cha Pemba waliopo Unguja waende kwao.
Sijui watu hawa wakiwemo maimamu wa sala ya Ijumaa (kama wanastahili kuitwa watu) wana lengo gani kwa kutoa kauli hii ya fitna na yenye kuhatarisha maelewano ya watu wa Visiwani.
Lakini kinachoshangaza na kusikitisha ni kuona mafatani hawa wenye kuhatarisha amani ya Zanzibar na watu wake wamenyamaziwa kimya na hawakuchukuliwi hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi lilisema linafanya uchunguzi, lakini kilichojitokeza ni kuudanganya umma kwa vile muda mefu umepita na hatujaona wahusika kuwajibishwa kisheria.
Sijui na tusiombe ikatokea kuwepo kundi la watu wajinga na wahuni kisiwani Pemba nao wakaanza kusema watu wenye asili ya Unguja wahame Pemba na kurudi kwao Unguja na karafuu ziliopo Pemba zisisafirishwe kwenda Unguja.
Kwa kweli Nahodha anafaa kupongezwa kwa kauli yake hii ya uzalendo na ya ujasiri ambayo bila ya shaka itawaudhi wahafidhina ambao hupenda kuona viongozi wa juu wa Serikali ya Zanzibar na Muungano wawe siku zote wanatoa kauli za kukuza malumbano badala ya kuendeleza maelewano.
Katika nchi ambayo vyombo vya habari vya umma huona vinao wajibu wa kuwaungaisha wananchi taarifa kama aliyoitoa Nahodha hupewa umuhimu sio kuitangaza tu, bali hata kuifanyia uchambuzi.
Lakini badala yake vyombo hivi vilivyopewa jina la Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) huona vigumu kutoa taarifa kama ya Nahodha au kumualika kwa mahojiano kuendeleza umoja wa wananchi.
Badala yake ZBC hualika mafatani wanaotoa maelezo ya uwongo na ubunifu juu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na kujisifia kuwa wametoa mchango mkubwa na kuwapaka matope wale waliokuwa mstari wa mbele kufanikisha Mapinduzi.
Fikiria unafiki wanaoutoa watu hawa kwa kuwaeleza vijana kwamba kabla ya Mapinduzi waliokuwa wanapata elimu Zanzibar ni Wahindi na Waarabu wakati wapo watu wengi, wakiwemo wale waliokuja kutoka Bara, walipata hata elimu ya kiwango cha juu.
Au ndio wanataka kutueleza wasomi wenye asili ya Waswahili (Waafrika) kama Marais wastaafu Sheikh Ali Hassan Mwinyi na marehemu Idris Abdulwakil ni wahindi na watu kama aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, marehemu Ali Khamis, Othman Sharif, Dk. Kingwaba Hassan na wengine wengi ni Waarabu?
Wote hawa na wengine wengi walipata elimu ya chuo kikuu miaka mingi kabla ya kufanyika Mapinduzi. Au zingatia unafiki wa hawa wazee mafatani wa kueleza kuwa hapo zamani wanawake wa Zanzibar walifagilishwa barabara ya mawe ya masafa ya maili 5 hadi 6 kwa kutumia matiti yao.
Sijawahi kusikia simulizi yoyote iliyoeleza kwamba hapo zamani akina mama wa Zanzibar au penginepo duniani walikuwepo wanawake wenye matiti ya chuma ambayo yaliweza kuhimili sulubu ya kufagia barabara ya mawe. Sijui hilo titi nalo lilikuwa na urefu gani.
Wakati umefika kwa wanasiasa wa Zanzibar wa vyama vyote, bila ya kujali utashi wao wa kisiasa, kujitokeza kama Nahodha kutoa kuali zitakaokuza maelewano na sio kutengana kwa watu wake ili utulivu uliopo uimarike na wajipatie maendeleo.Lakini wakati huo huo sio vyema, sio vizuri na ni hatari kuwafumbia macho na masikio wale wote wanaochochea siasa za chuki, fitna na uhasama.
Nchi hujengwa pale watu wake wa vyama mbali mbali vya siasa, dini, makabila na rika tofauti wanapokuwa wamoja na wenye kuelewana na kusikilizana katika mambo ya kheri na sio kugawana kama mafungu ya nyanya na kuangaliana kwa uadui na sio urafiki na udugu.
Hawa mafatani na wanaopalilia siasa za chuki wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wanapaswa kukumbuka angalizo la wahenga linalosema: Kila mchimba kisima huingia mwenyewe.
Ni vizuri hivyo visima vya maovu wanavyochimba wakavifukia haraka na kama wanataka kuchimba visima basi viwe vya maji safi na salama yatakayoleta faraja kwa wanaoyahitaji na neema kwa watu wa Zanzibar.
Tumuombe Mungu kwa pamoja aiokoe Zanzibar na aiepushe na mafatani wasiovitakia wema visiwa hivi ambavyo watu wake hapo kale walisifika kwa wema, hisani na ukarimu.
Chanzo : Tanzania Daima