HOTUBA YA UFUNGUZI WA WARSHA JUU YA UDHIBITI WA UTAKASISHAJI WA FEDHA HARAMU KWA MAAFISA UPELELEZI KUTOKA JESHI LA POLISI NA WAENDESHA MASHTAKA KUTOKA AFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA ZANZIBAR TAREHE 12 – 13 NOVEMBA, 2014
Imetolewa na Mhe. Said Hassan Said
Mwanasheria Mkuu Zanzibar.
1. Kaimu Kamisha, kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu,
2. Ndugu Washiriki kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Jeshi la Polisi Zanzibar,
3. Washiriki wa Warsha,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Alaykum.
Kwanza, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa kila kitu, Mola wa utukufu wote na mwingi wa Rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo kuhudhuria warsha hii muhimu tukiwa na amani, usalama na utulivu.
Natoa shukrani zangu za dhati kwa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu kwa kuandaa Warsha hii muhimu inayohusu Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu na kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi. Aidha, ninatoa shukrani kwa washiriki wote kwa jumla kwa kuitikia mwaliko na kuhudhuria warsha hii muhimu na kuwa tayari kutoa michango yenu ambayo ninaamini itaifanya nchi yetu iimarishe mfumo wa udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu.
Ndugu Washiriki, mabibi na mabwana,
Utakasishaji wa fedha haramu (money laundering) ni mchakato (process) wa makusudi unaofanywa na wahalifu katika jitihada za kuficha chanzo halisi cha pato linalotokana na uhalifu (proceed of crime). Vitendo vya uhalifu kama biashara haramu ya dawa za kulevya, rushwa, ujangili, ujambazi, biashara haramu ya kuuza watu na viungo vya watu, uuzaji haramu wa silaha, uharamia, ukwepaji wa kodi na kadhalika hufanywa na wahalifu kwa lengo la kupata fedha.
Fedha zinazopatikana kutokana na uhalifu mbalimbali ni fedha haramu ambazo watu hutafuta namna ya kuzifanya zionekane kuwa ni halali. Mchakato wa kuzihalalisha fedha hizi zionekane kuwa zinatokana na shughuli halali, ndio huitwa “Money Laundering” yaani Utakasishaji wa Fedha Haramu.
Tatizo la kuzitakasa fedha haramu lipo, kwa kuwa vitendo vya kihalifu vinavyowapatia pato haramu wahalifu kama biashara haramu ya dawa za kulevya, rushwa, ujangili, ujambazi, biashara ya watu na viungo vya watu, uuzaji haramu wa silaha, kukwepa kulipa kodi na uharamia bado vipo pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Serikali ya kupambana na wahalifu.
Ndugu Washiriki, mabibi na mabwana,
Utakasishaji wa Fedha Haramu ni tatizo kubwa ulimwenguni kote na katika jamii. Madhara yake kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama ni makubwa sana ikiwa ni pamoja na yafuatayo:-
· Kushusha hadhi ya nchi kimataifa (erosion of country’s integrity) na kusababisha nchi kutonufaika na mfumo wa fedha wa kimataifa,
· Kushusha imani ya wawekezaji na kusababisha uwekezaji kupungua na wawekezaji wapya kutotaka kuwekeza nchini. Kushamiri kwa uhalifu, wawekezaji huwa na hofu kuwa mitaji na mali zao havitakuwa salama,
· Kusababisha uhalifu kuendelea kushamiri kwani wahalifu wataendelea kufanya uhalifu; na kuendelea kunufaika na pato litokanalo na uhalifu.
· Kushusha hadhi ya mfumo wa fedha wa nchi (erosion of the integrity of the financial system).
· Kuharibu ushindani (ruin competitiveness) wa kibiashara kutokana na wahalifu kuwa na mitaji inayotokana na fedha haramu; na wafanya biashara halali kushindwa kuhimili ushindani.
· Kuhatarisha utawala wa Sheria na usalama (threaten peace, stability and rule of law) pale uhalifu unaposhamiri. Makundi ya uhalifu yanapojiimarisha hupata nguvu na kujaribu kudhibiti au kushindana na vyombo vya dola.
· Imani ya washirika wa maendeleo na jumuiya ya kimataifa hupungua na nchi huathirika kiuchumi.
Ndugu washiriki, Mabibi na Mabwana,
Ni dhahiri kuwa madhara niliyoainisha ni makubwa na yana athiri moja kwa moja jitihada za nchi yetu kufikia malengo yake ya maendeleo.
Kwa kuzingatia madhara makubwa ya utakasishaji wa fedha haramu, kiuchumi, kijamii, kiusalama na kisiasa, nchi mbalimbali duniani zikiongozwa na dhamira ya kukabiliana na uhalifu, makubaliano na mikataba ya Umoja wa Mataifa na itifaki za kikanda (UN Conventions and regional protocols), zimekubaliana kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na utakasishaji wa fedha haramu. Kila nchi inatakiwa kuwa na mfumo wa kisheria na wa kitaasisi (legal and institutional frame work) na kupambana na utakasishaji wa fedha haramu.
Mfumo wa kisheria ni pamoja na kutunga sheria zinazokidhi viwango vya kimataifa na kuridhia mikataba ya kimataifa. Mfumo wa kitaasisi ni pamoja na kuwa vyombo vya ushauri (advisory bodies) na vitengo vya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu (financial intelligence units) kwa ajili ya kutekeleza sheria za kupambana na utakasishaji fedha haramu. Vitengo vya udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu ni mihimili muhimu katika mfumo wowote imara wa kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu.
Ndugu Washiriki,
Nchi yetu kwa maana ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutambua kuwa tatizo la utakasishaji wa fedha haramu linahitaji udhibiti ili kupunguza madhara yake makubwa kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiusalama, ilitunga Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji wa Fedha Haramu mnamo mwaka 2006 (The Anti- Money Laundering Act); na kwa upande wa Zanzibar ilitunga Sheria ya Kudhibiti na Usafishaji wa Fedha Haramu na Mapato ya Uhalifu Nam. 10 ya mwaka 2009 (The Anti- Money Laundering and Proceeds of Crime Act) na hivyo kufanya utakasishaji wa fedha haramu kuwa ni kosa la jinai pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu Washiriki,
Nimeelezwa kuwa katika warsha hii mtapata fursa ya kupitia masuala mbalimbali kuhusu utakasishaji wa fedha haramu, mbinu wanazotumia wahalifu, hatua na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali mbalimbali na jumuiya ya kimataifa katika udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu na mambo yanayohusiana nayo. Ni dhahiri kuwa mmepata fursa adhimu ya kujadiliana na kueleweshana masuala haya muhimu ambayo kwa kiasi fulani ni mapya. Ninaomba itumieni fursa hii kwa umakini ili ilete tija kwenu binafsi na taifa kwa ujumla.
Ninaomba nisieleze kwa undani zaidi kuhusu masuala haya, niwaachie wataalamu matakaokuwa nao siku mbili hizi. Labda, nisisitize kidogo umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na suala hili. Ukweli kuwa tupo washiriki kutoka taasisi mbalimbali ni ishara na ujumbe wa kutosha kuwa tunahitaji kushirikiana kwa karibu kiutendaji ili mapambano haya yafanikiwe na kuinusuru nchi yetu dhidi ya uhalifu na hivyo kuiletea maendeleo inayostahiki.
Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana,
Ninaomba nikamilishe hotuba yangu kwa kueleza kuwa jitihada za Serikali za kupambana na utakasishaji wa fedha haramu zinaonesha mafanikio makubwa sana, kwani uhalifu unapungua nchini, wawekezaji wameendelea kuwa na imani na usalama wa mitaji na mali zao, mfumo wetu wa fedha unaaminika na unazidi kukua, kuimarika na hakuna makundi ya wahalifu yanayotishia utawala wa kisheria nchini. Hata hivyo tusibweteke na mafanikio hayo.
Serikali itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya utakasishaji wa fedha haramu yanaendelea ili kuinusuru nchi yetu na madhara yake ambayo ni ya kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kijamii; na hata athari za kimataifa.
Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana,
Kwa mara nyingine tena ninawashukuru wote walioandaa na kushiriki warsha hii muhimu na ninakutakieni uendeshaji na usikivu mzuri. Matumaini yangu ni kuwa mtashiriki vizuri; na taaluma mtakayoipata katika warsha hii mtaifanyia kazi na kuifikisha kwa wenzetu ambao tunafanya nao kazi lakini hawakubahatika kuhudhuria warsha hii ili kuongeza mwangaza katika jitihada za nchi yetu za kupambana na uhalifu.
Baada ya kusema hayo, sasa ninatamka kuwa Warsha hii imefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.