Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akipata maelezo kutoka kwa Afisa Tawala Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Makame Ali Ussi kuhusiana na mgogoro ulioibuka kati ya wananchi wa kijiji cha Kiomba Mvua, mkoa wa Kaskazini Unguja na mwekezaji anayejenga uwanja wa mchezo wa Golf. Kusho ni Mkuu wa Mkoa huo, Juma Kassim Tindwa na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'B', Khamis Jabir Makame.
Na. Khamis Haji, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema njia pekee itakayoweza kuleta suluhu ya mgogoro kati ya wananchi wa eneo la Kiomba Mvua na mwekezaji anayejenga uwanja wa mchezo wa gofu Kijijini hapo ni pande mbili hizo kukaa, pamoja na Serikali kutafuta njia za kuutatua.
Maalim Seif amesema hayo wakati alipofika katika eneo la mwekezaji huyo kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wananchi ya kulitembelea eneo hilo, baada ya wananchi hao kuwasilisha malalamiko yao kutokana na kuzuwiwa na mwekezaji kufanya shughuli za kiuchumi.
Maalim Seif amesema hakuna haja kwa wawekezaji na wananchi kuvutana, kwa sababu lengo la Serikali kukaribisha uwekezaji sio kuleta kilio na masikitiko kwa wananchi, bali ni kuwaletea neema wananchi hao na kuzidi kuimarisha maisha yao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Khamis Jabir Makame amesema kasoro zilizojitokeza na kufikisha hatua hiyo ni baada ya wananchi wa eneo hilo kukataa kutia saini makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande husika.
Naye Mwakilishi wa Viti Maalum, Mhe. Ashura Sharif Ali amesema wananchi wa Kiomba Mvua kimsingi wanakataa hatua ya kuzuiwa kufanya shughuli zao za kiuchumi katika eneo la bahari yao ya asili ya Nyanjale, ikiwemo uvuvi, upikaji na uanikaji wa madgaa, kwa sababu kazi hizo ndizo zinazowapatia riziki na kuwawezesha kuishi na familia zao.
Amesema eneo hilo kabla ya kutolewa kwa mwekezaji, lilikuwa likitumiwa kwa miaka mingi na wananchi wa Kiomba Mvua, Zingwe Zingwe, Fujoni na Kama katika shughuli mbaIi mbali za kujitafutia maisha, hivyo haikuwa busara kwa wananchi hao kuondoshwa bila ya kuwepo makubaliano maalum na kuzingatiwa hatma zao kimaisha.
Maalim Seif ameahidi kufuatuilia zaidi maamuzi yaliyotolewa awali na Kamati ya Baraza la Wawakilishi juu ya mgogoro huo, pamoja na makubaliano yaliyofikiwa ambapo wananchi hao walikataa kutia saini, ili ufumbuzi wa mzozo huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili uweze kupatikana.