Na Zuhura Juma, Pemba
Wakazi wa kisiwa cha Uvinje wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wamemuomba Mwakilishi wa jimbo la Gando, Mhe. Said Ali Mbarouk, kuzuia ujenzi wa hoteli katika kisiwa hicho, kwa hofu kwamba inaweza kuwa chanzo cha kuharibu mila, utamaduni na silka ya vijana wao.
Walisema hayo wakati walipokutana na Mwakilishi huyo ambae pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo hivi karibuni.
Mmoja wa wakazi hao Biwanu Ali Ussi, alisema utalii unaweza kusababisha vijana wao, hivyo hawako tayari kupokea mradi huo.
“Mimi binafsi nimeshuhudia hali hii, watalii wanapofika tu hapa, darasani wanafunzi wote hukimbia, kwa sababu wanawapa fedha na hili ni tatizo,” alisema mwakijiji huyo ambae pia ni mwalimu.
Simai Ali Simai (Karambisi) ambaye nae anaishi kisiwani hapo, alisema wameanza kupata hofu ya utalii kwa sababu wana hakika vijana wao wataharibika.
“Leo hii hawajajenga wanatembea tu watoto wote wanakimbia skuli, majumbani na kuwafuata, je wakijenga hoteli watalii wakaja kwa wingi watasoma tena, si watarejea ajira za watoto zinazokataliwa?,” alihoji.
Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo hilo, aliwataka wananchi hao kupunguza jazba na kukaa kwa amani, kwani kinyume na hivyo wanaweza kutofautiana miongoni mwao akisema lengo la serikali ni kuimarisha sera ya utalii kwa wote.
Aliwaahidi wakazi wa kisiwa hicho kwamba atawapeleka ngazi zote za serikali zinazohusika na shughuli hizo, ikiwa ni pamoja na Mkuu wa mkoa huo, Mkuu wa wilaya, Kamisheni ya Utalii,
Mamlaka ya ardhi pamoja na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), ili kuwasilisha malalamiko yao.