Na Mwandishi wetu
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimevitaka vyombo vya usalama wa taifa, polisi na mahakama kushirikiana katika kupambana na wahalifu na wote wanaohusika katika kutekeleza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa watoto nchini.
Kauli hiyo imetokana na idadi ya kesi za ukatili na utekwaji watoto wa kike zinazoripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto kwenye vituo vya polisi nchini kuongezeka.
Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2014 idadi ya kesi za ukatili wa kijinsia kwa watoto kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 519 hii ni pamoja na mikoa mitatu ya kipolisi yaani Kinondoni, Temeke na Ilala, ikifuatiwa na Zanzibar 219 (Unguja magharibi na kusini), Shinyanga 69, Mara 62, Tabora 55, Morogoro 36, Kagera 32 na mkoa wa Pwani 20.
Katika taarifa za vitendo vya kikatili kwa watoto matukio yaliyojitokeza ni yale ambayo yanahusisha vitendo vya ubakaji, ulawiti, mateso, kutelekezwa kwa watoto, utekwaji nyara na kupotea kwa watoto wa kike.
Taarifa ya TAMWA ilisema hivi karibuni mkoani wa Dar es Salaam zililipotiwa taarifa za watoto watatu waliokuwa wakisoma skuli ya msingi Miembeni, Vingunguti waliopotea katika mazingira ya kutatanisha.
Taarifa hizo zilitolewa na wananchi waishio maeneo ya Mbezi kwa Msuguri, Mbezi Msigani na kwamba vitendo vyengine vya kikatili vimeripotiwa katika wilaya ya Kinondoni na Temeke.
TAMWA katika mradi wake wa Kujenga na Kuimarisha Usawa wa Kijinsia na Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia (GEWE II) kupitia kituo chake cha Usuluhishi cha (CRC), kwa kipindi cha mwezi Oktoba mwaka huu kimepokea matukio 16 ya kikatili kwa watoto ambapo yameongezeka kutoka matukio tisa ya mwezi Septemba.
Aidha, kwa ujumla katika kipindi cha mwaka 2014 idadi ya matukio hadi sasa yameongezeka kuwa 66 ikilinganishwa na ya mwaka 2013 ambapo taarifa za matukio zilikuwa ni 41.