Na Ally Ndota
Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, leo anatarajia kuanza ziara katika wilaya zote 12 za mikoa sita ya kichama ya Unguja na Pemba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar, Dk. Shein, ataanza ziara hiyo kwa kutembelea wilaya ya Mjini.
Lengo kuu la ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, ni kubadilishana mawazo na uzoefu juu ya masuala ya kisiasa, ujenzi na uimarishaji wa chama hicho na viongozi wa mashina wa wilaya ya hiyo.
Atakamilisha ziara yake hiyo, mkoani humo Novemba 19, ambapo atazuru wilaya ya Amani na siku inayofuata, atatembelea wilaya ya Dimani, Mkoa wa Magharibi.
Atahitimisha ziara yake hiyo Disemba 4, mwaka huu, ambapo atabadilishana mawazo kuhusu uimarishaji wa chama na mabalozi wa wilaya ya Mkoani, mkoa wa kusini, Pemba.
Katika ziara hiyo, atafuatana na viongozi mbali mbali wa chama hicho, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM- Zanzibar, Vuai Ali Vuai pamoja na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC Zanzibar.