STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 17 Novemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema anaheshimu utaratibu wa kupata wagombea katika chama chake hivyo kamwe watu wengine wasimsemee kuhusu suala hilo.
Dk. Shein amefafanua kuwa wako watu wanaopita huku na kule kueleza kuwa yeye hatagombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao jambo ambalo amesema yeye hawajawahi kulitamka.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na viongozi wa mashina na wa maskani wa Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Mjini kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Salama wa hoteli ya Bwawani mjini hapa,
Dk. Shein alieleza kuwa hajawahi kuzungumza na mtu yo yote juu ya suala hilo na kuhoji “kwa nini watu wengine wanisemee wakati mimi mwenyewe nipo”.
Alifafanua kuwa yeye anaelewa vyema utaratibu wa chama chake kuhusu suala hilo na kusisitiza kuwa si mgeni wa mambo ya chama kwani amekulia katika chama hicho tangu akiwa mdogo.
“Niliingia Chama cha Afro Shirazi nikiwa kijana mdogo na nimekuwa nikikitumikia tangu wakati huo na hata nilipata kufukuzwa skuli nikiwa darasa la nne kwa sababu ya kujihusisha kwangu na Chama hicho hivyo sikurukia jahazi” Dk. Shein alieleza.
Akionesha kukerwa na jambo hilo, Dk. Shein alisema anashangazwa na vitendo vya baadhi ya watu kupita mitaani na kuzungumzia habari zake huku wakielewa fika kuwa wanachokifanya ni kitu kisichofaa.
“Msivamie mambo, hayo mnayopita mkiyasema hayawasadii kitu, kama hamyajui mimi mwenyewe nipo niulizeni lakini sio kusema yasiyostahiki” Dk. Shein alieleza.
Alisema ni muhimu kwa viongozi kuheshimiana na kwamba yeye amekuwa akimheshimu kila mtu mkubwa kwa mdogo na kuongeza kuwa kama wako walio na hoja dhidi yake basi wasubiri wakati wa uchaguzi utakapofika.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema kuingizwa suala la mashina na maskani katika katiba ya Chama cha Mapinduzi ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa mashina na maskani zinaendelea kuwa nguzo muhimu katika mustakbala wa chama hicho.
“Tunathamini mchango wenu ndio maana viongozi wa mashina(mabalozi) wameingizwa katika Katiba ya chama ili washiriki katika mchakato wa kuwapata wagombea wa chama chetu wakati wa uchaguzi” alisema.
Kwa hivyo aliwaeleza viongozi wa mashina na maskani katika mkutano huo kuwa chama hicho kinathamini sana mchango wao katika kuimarisha chama hicho huku akisisitiza kuwa mashina na maskani ndio nguzo ya ushindi wa CCM.
Aliongeza kuwa maskani “ndio nguzo ya ushindi wa chama cha Mapinduzi” na ndio maana wengine wamekuwa wakizipinga na hata kushiriki kuzihujumu.
Kwa hivyo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa maskani hizo zinakuwa kitovu cha upendo na mshikamano miongoni mwa wanachama na wapenzi wa chama hicho ili kuimarisha nguvu za CCM na kukihakikishia ushindi katika changuzi zijazo.
Katika mkutano huo uliojumuisha viongozi zaidi ya elfu moja, Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliwataka viongozi hao kuthamini wajibu wao wa kuyatetea Mapinduzi ya mwaka 1964 pamoja na Muungano kwa kuwa hizo ni matokeo ya nguvu za viongozi na wazazi wao.
“lazima tutanabahi wakati wote kuwa CCM ndio mlinzi wa Mapinduzi na Muungano. Tusibabaishwe wala kuhadaika na chochote wala tusijaribu kuzembea katika hili” Dk. Shein alitanabahisha.
Alifafanua kuwa tukio la kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 lilikuwa la lazima na ndio lililoiletea heshima Zanzibar hivyo ni wajibu wa kila mwana CCM na mzazibari kuyalinda.
Aliwahakikishiwa viongozi hao kuwa pamoja na changamoto nyingi zinazokikabili chama hicho lakini kinajidhatiti kuwapatia viongozi hao nyenzo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Ukosefu wa nyenzo isiwe jambo la kutufanya tusinzie... tutazitafuta na tutahakikisha tunawapatia ili mkitapatie ushindi chama chetu” Dk. Alieleza.
Akizungumza kabla ya mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alimpongeza Dk. Shein kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM na kumhakikishia wana CCM wataendelea kumuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Ilani hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilya Mjini Bwana Juma Fadhil aliwataka wana CCM na wananchi wa Zanzibar kutofautisha mambo ya ukweli na mapenzi ya mtu kwa mtu na kuwafafanulia kuwa katika suala la Katiba ni busara kufuata ukweli ulioambiwa badala ya kuangalia ukweli huo umesemwa na nani.
“Tusikilize ukweli katika suala la Katiba iliyopendekezwa sio kuhoji ukweli kwa kuwa tu umesemwa na mtu usiyempenda kwani kufanya hivyo tutakuwa tunafanya makosa” alisema Mwenyekiti huyo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822