Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesisitiza haja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa ya kutambua mchango unaofanywa na serikali wa kukabiliana na vitendo vya kikatili dhidi ya wananchi wake wenye matatizo ya ulemavu wa ngozi ( albino)
Wito huo wa Tanzania umetolewa mapema wiki hii ( Jumanne) wakati Wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa walipopitisha kwa kupiga kura, Azimio linalotaka Juni 13 ya kila mwaka iwe ni siku ya Kimataifa ya kuwatambua watu wenye ulemavu wa ngozi.
Balozi wa Somalia kutoka Geneva ambako ndiko chimbuko la Azimio hilo, ndiye aliyeongoza mchakato mzima wa uwasilishaji wa azimio katika Kamati ya Tatu inayohusika na masuala ya Haki za Binadamu, Jamii na Utamaduni.
Tanzania ikiwa ni mjumbe wa Kamati hiyo ya Tatu, pamoja na kuunga mkono uwepo wa siku ya Kimataifa kwaajili ya walemavu wa ngozi. Ilibani mapungufu kadhaa yakiwamo ya kiufundi katika eneo zima la uwasilishwaji wa Azimio lenyewe na kubwa zaidi, Azimio halikuwa linatambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kulishughulikia tatizo hilo.
Kutokana na mapungufu hayo na namna azimio lilivyowasilishwa, Tanzania ilipendekeza kwa wajumbe wa Kamati nyongeza ya vipengele kikiwamo kinachotambua mchango na juhudi za serikali
Aidha pamoja na pendekezo hilo, Tanzania pia ilishauri kuwa ili Azimio hilo liwe na tija zaidi kwa walengwa, lakini pia kama sehemu ya uelimishaji jamii juu ya matatizo yanayowakibili watu wenye ulemavu wa ngozi, ikataka pawe pia na kipengele kinachoiagiza Jumuiya ya Kimataifa kuziwezesha na kuzisadia nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo hilo.
“ Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatuna tatizo na dhana nzima ya ujumbe na umuhimu wa Azimio hili. Nchi yetu ni kati ya nchi zenye idadi kubwa ya watu ambao wana ulemavu wa ngozi. Ni kundi hili la jamii linakumbana na matatizo mengi yakiwamo kufanyiwa vitendo vya kikatili na kunyanyapaliwa n ahata kupoteza maisha. Amesema mwakilishi wa Tanzania
Na kuongeza kwamba, pamoja na ukubwa wa tatizo na changamoto zake, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajitahidi kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na udhalimu na ukatiliwanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tanzania imesisitiza kwamba haitoshi kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu wa ngozi bila ya kuwa na mipango na mikakati madhubuti na yenye tija ambayo kwayo italenga zaidi kuwasaidia walengwa na serikali.
Baada ya majadiliano na ushawishi mkubwa Tanzania imefanikiwa kuingiza katika Azimio hilo kipengele ambacho Jumuiya ya Kimataifa inatambua juhudi na mchango wa serikali katika eneo hilo.
Azimio limepitishwa kwa kupigiwa kura 160 za ndiyo, na 16 hazikufungamana na upande wowote.