STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29 Novemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali imeamua kuagiza vifaa vipya vya ujenzi wa barabara ili kuhakikisha kuwa miradi yote ya barabara iliyopangwa iweze kutekelezwa na kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka ujao.
Akizungumza na viongozi wa mashina na wenyeviti wa maskani za Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kaskazini ‘B’ leo, Dk. Shein amesema serikali inafanya hivyo ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara kwa kuwa hivi sasa vifaa vilivyopo haviwezi kutekeleza mradi zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.
“Tunatazwa na mambo madogo madogo lakini fedha tunazo za kutosha kufanya kazi hiyo hivyo tumeamua kuagiza vifaa zaidi ili kuongeza kasi kwa kutekeleza miradi zaidi ya moja kwa wakati mmoja hivyo matarajio yetu ni kukamilisha miradi hiyo kwenye mwezi Agosti 2015” Dk. Shein alifafanua.
Kwa hivyo aliwahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kuwa barabara za wilaya hiyo zilizomo katika mpango wa serikali zitajengwa katika kipindi hicho hivyo wanachotakiwa kwao ni kufanya subira.
Kuhusu suala la mgogoro kati ya kiwanda cha sukari Mahonda na wananchi ambao viongozi hao waliuzungumzia, Dk. Shein aliwaeleza kuwa suala hilo linashughulikiwa na serikali kwa umakini mkubwa na kufafanua kuwa tatizo hilo linachochewa na baadhi ya viongozi ambao alisema serikali itawashughulikia ipasavyo wakati utakapofikia.
“Lipo tatizo lakini pia tunafahamu kuwa wapo baadhi ya viongozi wanaochechea mgogoro huo hivyo tutawachukulia hatua kali wote wanaoshiriki katika kukuza mgogoro huo” Dk. Shein alisisitiza.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi katika mikoa na wilaya zote Unguja na Pemba kwa kushirikiana kikamilifu na serikali katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM na hatime kupata mafanikio makubwa.
“Tumeshikamana sote katika mikoa yote ya Zanzibar kutekeleza Ilani ya chama chetu. Ni kazi kubwa lakini ndio itakayotupeleka tena kwa wananchi kuwaomba waichague tena CCM katika uchaguzi ujao” alisema Dk. Shein.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, muda uliobaki sasa hadi uchaguzi ujao utekelezaji wa Ilani hiyo utaendelea kufanyika huku changamoto mbali mbali zinazokabili utekelezaji wake zikitafutiwa ufumbuzi kwa mfano ununuzi wa vifaa vipya kwa ajili ya kukamilisha miradi ya barabara.
Aliwataka viongozi na wananchi kutokuwa na wasiwasi na uendeshaji wa serikali kwa amekuwa akiiongoza mujibu wa sheria na kwa umakini mkubwa na kusisitiza kuwa haki inatendeka kwa kila mwananchi.
“Naongoza serikali kwa mujibu wa Katiba na bila ya ubaguzi au kumchukia mtu na huo ni wajibu wa kiongozi kumpenda kila mwananchi wake kwani akifanya kinyume chake kiongozi anakosa sifa” Dk. Shein aliwaambia viongozi hao.
Hata hivyo aliongeza kuwa hilo halimfanyi kwenda kinyume na chama chake au kwenda kinyume na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa yeye anawajibika kwa chama chake.
“Nahakikisha kuwa shughuli za serikali zinatekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa progamu zake ambazo zimezingatia Ilani ya Uchaguzi na ndio maana nimeweka utaratibu wa kutathmini utekelezaji kila baada ya robo mwaka” alisema Dk. Shein akiimaanisha mikutano ya Bangokitita ambayo hufanyika kila baada ya robo mwaka ya mwaka wa fedha.
Akimkaribisha Dk. Shein katika mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Bravo huko Kiwengwa, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwaeleza viongozi hao kuwa wasiwasikilize watu wanaojiita Kamati ya Maridhiano kwa kuwa wanajipa sifa wasizostahili kwa kudai kuwa wao ndio chimbuko la Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa chimbuko lake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliahidi wakati alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano mwezi Disemba 2010 kuwa suala la Zanzibar lazima litafutiwe ufumbuzi wa kudumu”Naibu huyi alieleza na kuongeza kuwa baada ya kauli hiyo alitumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa CCM kuznisha majadiliano kuhusu suala hilo.
Katika maelezo yake, Naibu Katibu Mkuu huyo alihimiza pia wajumbe wa vikao mbalimbali vya chama hicho kuhudhuria kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na kwamba viongozi wanapaswa pia kuzingatia suala la mahudhurio ya vikao katika kuwatathmini wajumbe hao wanapoomba tena nafasi za uongozi na kuchaguliwa.
Dk. Shein amemaliza ziara hizo kwa wilaya za Unguja na anatarajiwa kuanza ziara kama hizo katika wilaya nne za Pemba kuanzia Jumatatu ijayo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822