Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Viongozi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja akiwa katika jitihada zake za kuimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa huo,(kulia) Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, na wa kwanza (kushoto) Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa Khadija Hassan Aboud akifuatiwa na Mwenyekiti wa CCM Kaskazini A Unguja Ali Makame Khamis, sambamba na jitihada hizo leo anatarajiwa kuanza kuzungumza na Viongozi mbali mbali wakiwemo Mabalozi na Wenyeviti wa Maskani wa Chama hicho katika Mikoa ya Pemba. [Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 30.11.2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewataka vijana kuheshimu jitihada za wazee na viongozi wao sambamba na maendeleo yaliopatikana hapa nchini ambayo yametokana na Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Hayo aliyasema leo huko Chaani Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja mara baada ya kulikagua Tawi la CCM la Chaani Mchezashauri ambapo alipata fursa ya kusalimiana na WanaCCM na wananchi wa eneo hilo na viunga vyake.
Katika nasaha zake Dk. Shein alisema kuwa vijana wanadhima kubwa ya kuheshimu maendeleo yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu wazee na viongozi wao wa nchi na kuwataka vijana wasihadaiwe.
Alisema kuwa vijana wanajukumu kubwa la kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 pamoja na kusisitiza haja ya kuutunza na kuulindda Muungano uliopo ambao unahistoria na mafanikio makubwa na kuwashangaa wanaoupinga Muungano huo.
“Vijana msidharau watu, msiwadharau wazee na viongozi wa nchi hii hakuna sababu ya kutukana watu heshimu na wewe uheshimiwe... watu hawajui watokako..mtu kwao ndio ngao”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa jambo lolote lililoasisiwa na ASP kuna kila sababu ya kuliendeleza na kueleza kuwa watu wa Chaani pamoja na watu wa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja wanaheshima kubwa katika ukombozi wa nchi hii hivyo ni lazima kuwajengea heshima.
Kutokana na hayo, Dk. Shein aliwataka wazee na wazazi kuwaeleza vijana historia ya nchini hii sambamba na juhudi zilizofanywa na wazee hao katika kuiokomboa kwa kufanya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na hatimae hivi leo wananchi wanajitawala wenyewe.
Akieleza kuhusu historia ya Tawi hilo ambalo ni miongoni mwa Matawi ya mwanzo yenye historia kubwa hapa nchini, Dk. Shein alisema kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa na CCM kwa kushirikiana viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho katika kuhakikisha Matawi yake yote ya Unguja na Pemba yanaimarika na kwenda sambamba na uimara wa chama hicho.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa ASP ndio chama kilichopigania ukombozi wa Zanzibar hivyo kuna kila sababu ya kuheshimu juhudi zake zikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Matawi ulioanzishwa wakati huo wa kudai uhuru.
Nao WanaCCM wa Tawi hilo pamoja na viongozi wa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja walitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa juhudi zake katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2010-2015 sambamba na hatua anazozichukua katika kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar.
WanaCCM hao wameeleza kuridhishwa kwao na uongozi wa Dk. Shein na kuahidi kuendelea kumuunga mkono katika kuiletea nchi maendeleo pamoja na kukiimarisha chama chao ili kiendelee kushika hatamu huku wakieleza kuunga mkono Katiba iliyopendekezwa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk