Na Kija Elias, Moshi
Imeelezwa uwepo wa fedha nyingi bandia nchini umechangia kupunguza thamani ya fedha halisi na kusababisha mfumuko wa bei.
Hayo yaliemwa na Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Arusha,Said Chiguma, wakati wa kikao cha dharura cha Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Kilimanjaro (RCC),ambapo alisema nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la uingizwaji wa fedha bandia jambo, ambalo limesababisha baadhi ya fedha hizo kuingizwa kwenye mzunguko huo.
Alisema miongoni mwa mikoa iliyoathirika na uwepo wa fedha hizo ni pamoja na Arusha ambao unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya noti bandia za shilingi 10,000 kwa kuwa na jumla ya noti bandia 102 na noti za shilingi 5,000 kwa kipindi cha Julai 2013 hadi Juni 2014.
Alisema mkoa ambao unafuatia ni Manyara ambao una noti za shilingi 10,000 zinazofikia 84.
Alitoa rai kwa wananchi wa kanda ya kaskazini kuwa makini pindi wanapopokea fedha hususani nyakati za usiku.
Alisema takwimu hizo zinatokana na matukio yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi ambapo kwa upande wa fedha bandia zilizopatikana kutoka katika benki za biashara kwa mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na jumla ya noti bandia 426 ambayo sawa na asilimia 55.9.
Mkurugenzi wa Benki ya Wananchi Mwanga (MCB), Abi Mangia, alisema wakulima wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa elimu ya ujasiriamali wa kilimo hali ambayo imekuwa ikirudisha nyuma jitihada za wakulima hao kujikwamua kiuchumi.