Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema uteuzi wa Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Assad ataapishwa leo saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi wake, Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Ludovick Utouh, ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.
Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana shahada ya uzamivu wa uhasibu (PhD in Accounting)kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na shahada ya uzamivu katika udhibiti wa fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.
Pia ana stashahada ya kitaaluma ya uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na shahada ya biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1988.
Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad ana uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi.
Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 - 2014); ni Rais na mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012; na ni mjumbe wa bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika uteuzi huo, Rais Kikwete alisema ana imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu wake utamwezesha kutekeleza vyema majukumu ya nafasi hiyo muhimu katika utawala bora.