STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 01 Disemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema anaamini kuwa Tume ya Utumishi Serikalini inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kama kuna malalamiko dhidi yake Serikali itafuatilia.
Akizungumza na viongozi wa mashina na wenyeviti wa maskani wa wilaya ya Wete leo, Dk. Shein alisema kuwa kuanzishwa kwa Tume ya Utumishi ni sehemu ya utekelezaji ahadi ya Chama cha Mapinduzi ya kuimarisha utawala bora.
“Ni ahadi ambayo tuliiweka hivyo tulipounda serikali tulilazimika kuunda Wizara hii kubwa na taasisi zake ambazo zinatekeleza suala hilo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa”, Dk. Shein alieleza.
Alisema yeye binafsi haamini kuwa Tume za utumishi zinapendelea bali zinatekeleza sheria ya utumishi wa umma ambayo wananchi wengi hivi sasa hawajaielewa vyema.
“Kuundwa kwa Taasisi hizi isiwe tatizo kwetu, haya ni mambo yetu wenyewe tuliyoyaanzisha kwa mujibu wa Katiba yetu na kama kuna watendaji hawatekelezi majukumu yao ipasavyo ni wajibu wetu kuwawajibisha” Dk. Shein alisema.
Katika mkutano huo baadhi ya viongozi walilalamikia mfumo wa ajira serikalini hivi sasa kwa madai kuwa kuna upendeleo.
Wakati huo huo Dk. Shein aliwataka viongozi hao kutokuwa na wasi wasi kuhusiana na suala la amani na utulivu katika uchaguzi mkuu ujao, akiwahakikishia kuwa huu si wakati tena wa kutishana na wasibabaishwe na watu waliozea kuwatisha wananchi hasa wakati wa uchaguzi.
“msiwe na wasiwasi, tutaweka ulinzi wa kutosha wakati wa uchaguzi, wakati wa kutishana ulikomeshwa na Mapinduzi ya mwaka 1964” na kuwataka wananchi wasikubali kutishwa kwa kuwa watu hao “hawana mamlaka ya kufanya hivyo” Dk. Shein alieleza.
Aliongeza kuwa hivi sasa nchi inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba hakuna mwananchi aliye juu ya sheria hivyo kila mmoja anapaswa kufuata sheria na kinyume chake sheria zitafuata mkondo wake.
Alirejea ahadi ya serikali ya kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa haki na huru na kwamba uimarishaji wa ulinzi na usalama ni sehemu ya maandalizi hayo.
Alisema wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Jeshi la Polisi imebuni sera ya ulinzi shirikishi na kupata mafanikio makubwa katika suala zima la ulinzi wa usalama wa raia na mali zao, viongozi hao wa CCM nao wanaweza kubuni mbinu zitakazosaidia ulinzi ndani ya chama hicho dhidi ya watu wasiopendelea maendeleo yake.
Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Jamhuri mjini Wete, Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwataka wana CCM kuendeleza kasi ya kuimarisha chama chaoa ili kuwahakikishia ushindi katika uchaguzi ujao.
“Tuendelee kujiimarisha ili kuendeleza historia ya chama chetu ya kushinda kila uchaguzi ” Dk. Shein alisisitiza.
Mapema akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa alisifu utekelezaji wa Ilani katika mkoa huo na kueleza kuwa matokeo ya utekelezaji huo umeleta mabadiliko katika maisha ya kila siku ya wananchi.
“Ujenzi wa barabara mbalimbali katika mkoa wetu umeleta mabadiliko katika hali za maisha ya wananchi ikiwemo makaazi kwa wananchi kuhamaiska kujenga nyumba bora” Mzee Mberwa alieleza.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwaeleza viongozi hao kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa kama vile suala la Katiba inayopendekezwa.
Alisema upinzani walitaka Katiba ambayo itavunja muungano badala ya kuimarisha na ndio maana wamekuwa wakitumia muda mwingi kupotosha wananchi kwa mambo yasiyo ya msingi.
Dk. Shein anatarajiwa kuendelea na ziara yake hiyo ya kichama kesho kwa kuzungumza na viongozi wa chama hicho katika wilaya ya Micheweni.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822