Na Khamis Amani
Mahakama ya Rufaa Tanzania kanda ya Zanzibar, imeanza rasmi kikao chake cha wiki mbili kwa kusikiliza mashauri mbali mbali ya jinai na madai yaliyowasililishwa mahakamani hapo.
Mahakama hiyo yenye jopo la Majaji watatu, inatarajia kusikiliza rufaa na maombi 21 ambayo maamuzi na hukumu zake zinatarajiwa kutolewa Disemba12 mwaka huu.
Kikao hicho kinachofanyika mahakama kuu Zanzibar iliyopo Vuga mjini Unguja, ambapo kabla ya kuanza rasmi kazi zake kimefunguliwa kwa gwaride kutoka kwa askari wa jeshi la Polisi wa kitengo cha kutuliza ghasia (FFU) lililofanyika nje ya jengo la mahakama kuu.
Majaji wanaotarajia kusikiliza kesi hizo ni Jaji Kimaro, Jaji Luanda pamoja na Jaji Mjasiri ambao kwa pamoja walianza kusikiliza shauri la madai lililofunguliwa na Machano Khamis Ali pamoja na wenzake 17 dhidi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Kwa mujibu wa Francis Jacob Kabwe, Naibu Msajili wa mahakama ya Rufaani Tanzania, jumla ya mashauri 21 yamewasilishwa mahakamani hapo yakiwemo maombi manane ya madai, rufaa nane za madai, ombi moja la jinai pamoja na rufaa nne za jinai.
Mashauri yote hayo yamewasilishwa mahakamani hapo baada ya wahusika wake kutoridhika na maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu ya Zanzibar na kuamua kupanda ngazi katika mahakama hiyo kwa mujibu wa sheria ili kuona haki inatendeka.
Kikao cha mahakama ya rufaa kanda ya Zanzibar kinafanyika mara moja kwa mwaka kwa kusikiliza na kutoa maamuzi ya kesi na maombi mbali mbali ya jinai na madai baada kutoridhika na maamuzi yanayotolewa na mahakama kuu ya Zanzibar.