Na Augusta Njoji, Dodoma
Watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga lori kwa nyuma wakati ikitaka kuzpita gari zilizokuwa mbele yake.
Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 12:30 jioni katika eneo la njia panda ya NARCO barabara kuu ya Morogoro-Dodoma wilayani Kongwa.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa,David Misime, alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T 213 DAR Toyota Mark X ambalo lilikuwa likiendeshwa na Hassan Hussein (35), mkazi wa Dodoma likiwa na abiria wanne wakitokea Morogoro wakielekea Dodoma.
Alisema gari hilo liligonga kwa nyuma gari lenye namba za usajili T 963 BRC Leyland Daf lililokuwa na tela lenye namba T708 ASP likiendeshwa na Tumaini Josia (23) mkazi wa Mbagala rangi tatu mkoani Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu wawili pamoja na majeruhi watatu.
Aliwataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni John Mmasi maarufu kwa jina la Matei (32),mmiliki wa Matei Lounge ambaye alifariki njiani alipokuwa akikimbizwa hospitali ya rufaa Dodoma na Joshua Oguda(32) wakili wa kujitegemea aliyefariki akiwa anaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa Dodoma.
Kwa upande wa majeruhi ni Bossi Ngasa (28), Juma Zuberi (23), Hassan Hussein(35) aliyekuwa dereva wa gari dogo ambao wote wamelazwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma wakiendelea na matibabu.
Misime alisema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari dogo kutaka kuzpita gari zilizokuwa mbele bila kuchukua taadhari.