Na Waandishi wetu
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, amesema kuwa kazi ya urais siyo jambo la kushauriwa au kuombwa, bali kwa mhusika kujipima kama anaweza kutekeleza jukumu hilo kwa kuweka maslahi ya umma mbele kuliko kutafuta heshima na mali nyingine.
Kificho aliyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa NIPASHE mjini Zanzibar hivi karibuni na kutaja sifa kuu mbili anazostahili kuwa nazo Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ajaye.
Alifafanua sifa hizo kuwa mtu mwenye nia thabiti ya kuwa tayari kuchukua, kulimudu na kuwafanyia vyema Watanzania.
Pili, ashirikiane kwa karibu na wenzake kutambua kuwa akifanikiwa kwenye jambo husika siyo yeye pekee bali waliofanikiwa ni wananchi, ikiwa ni pamoja na kusahau atapata nini bali atawafanyia nini watu anaotarajia kuwaongoza.
Alisema ni lazima rais atambue kuwa jukumu ya kuongoza serikali siyo kuongoza Baraza la Mawaziri pekee, bali ndiye mwenye dhamana zote, na atambue kwamba wengine wakiboronga katika mihimili mingine yeye ndiye wa kuulizwa.
“Viongozi tuelewe unataka kuchukua jukumu la kuongoza na siyo kufikiri katika kazi hiyo nitapata heshima bali jiulize nini utawafanyia watu wako, kama ni heshima utaipata kutokana namna unavyowafanyia watu, kama ni sifa ni kutokana na namna unavyotekeleza majukumu yao, kama thawabu ni kwa namna unavyotimiza wajibu wako na kuwatendea watu,” alisema na kuongeza:
Kificho aliyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa NIPASHE mjini Zanzibar hivi karibuni na kutaja sifa kuu mbili anazostahili kuwa nazo Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ajaye.
Alifafanua sifa hizo kuwa mtu mwenye nia thabiti ya kuwa tayari kuchukua, kulimudu na kuwafanyia vyema Watanzania.
Pili, ashirikiane kwa karibu na wenzake kutambua kuwa akifanikiwa kwenye jambo husika siyo yeye pekee bali waliofanikiwa ni wananchi, ikiwa ni pamoja na kusahau atapata nini bali atawafanyia nini watu anaotarajia kuwaongoza.
Alisema ni lazima rais atambue kuwa jukumu ya kuongoza serikali siyo kuongoza Baraza la Mawaziri pekee, bali ndiye mwenye dhamana zote, na atambue kwamba wengine wakiboronga katika mihimili mingine yeye ndiye wa kuulizwa.
“Viongozi tuelewe unataka kuchukua jukumu la kuongoza na siyo kufikiri katika kazi hiyo nitapata heshima bali jiulize nini utawafanyia watu wako, kama ni heshima utaipata kutokana namna unavyowafanyia watu, kama ni sifa ni kutokana na namna unavyotekeleza majukumu yao, kama thawabu ni kwa namna unavyotimiza wajibu wako na kuwatendea watu,” alisema na kuongeza:
“Jukumu hilo ni zito mbele ya binadamu na zaidi mbele ya Mungu, sina uhakika hata kidogo kama uzito huo naweza kuumudu hata chembe na kwa sababu ya uzito huo sitegemei wenzangu wanishauri kufanya jambo kama hilo, kama ni vizuri namshukuru Mungu, kama nimekosea namuomba anisamehe, nadhani imetosha kwa utumishi niliyofanya kwenye nafasi ya Spika, mahakama na serikalini.”
Alisema hana hakika kama sifa za kuwa rais anazo na wala hatarajii kugombea urais wa nchi au Zanzibar kwa kuwa amejipima na kuona kuwa nafasi hiyo haiwezi, jambo ambalo linapaswa kufanywa na viongozi wengine.
“Mambo ya siasa kwa ujumla wake, hata uwakilishi sikuwahi kuomba, ilikuwa ni ‘formality’, lakini nilishauriwa na watu kwamba tunahisi ungefanya hivi ungetusaidia, niligombea uwakilishi na nilipoangushwa mwaka 1995, sikuwahi kuomba nafasi ya uspika zaidi ya chama changu kunishauri ukiomba utaweza kutusaidia,” alisema.
“Kwa tabia yangu huwa siombi uongozi ila kuna watu wananishauri kuchukua uongozi, kwa uzito wa jukumu la urais sina nia ya kuomba na sitategemea wenzangu kunishauri hivyo,” alisema.
“Nitakuwa katika nafasi nzuri ya kushauri wenzangu wenye kuweza kufanya vizuri, hisia zao wachanganye na hizi…jukumu hili ni zito sana nazingatia dhamana kuliko nitapata nini, mengine yote kama kupata kitu ni wizi mtupu,” alisema.
UMRI WA URAIS
Alisema sifa za urais zitapatikana kwa mtu mwenye umri wa kati kwa kuwa atakuwa na uwezo wa kuvumilia na aliyekomaa na kwamba umri mkubwa nao unategemea na mtu kwani wapo ambao wanashindwa kusimamia maisha yao licha ya ukomavu na elimu kubwa.
Alisema kuna baadhi ya vijana wamekomaa kiakili, wana uvumilivu, ukomavu, wamesoma vizuri, na wanaweza kuongoza na hata urais, lakini wenye kufaa ni wenye umri wa utu uzima ambao ni wenye utulivu, busara, usikivu, mwenye uwezo wa kupima anachoelezwa kabla ya kuamua kwa faida ya unaowaongoza.
RUSHWA
Alisema kinachoisumbua Tanzania ni kuweka ubinafsi mbele na kuacha kufanya majukumu ya msingi kwa kiongozi wa umma. Ameonya kwamba tamaa ikiwa kubwa lazima itatafuta pa kufanya ufisadi, uporaji na kuiba.
“Hili linasikitisha sana, mara nyingi ninapozungumza na wenzangu nawaambia siasa imekwisha, siasa ninayoijua ni utumishi na ndiyo maana sipendi kusema mimi ni fulani bali mtumishi wa wananchi,” alisema.
Alisema kwake maslahi yanakuja baada ya kazi na kwamba hutegemea ujira kwa mujibu wa kazi aliyofanya.“Siyo jambo jema unapopewa kazi ukajiangalia mwenyewe na watu wa familia yao bila kuzingatia mislahi ya Taifa au ya wengi katika jamii, ni wajibu wetu kuzingatia masuala ya familia za wanaotutegemea, lakini isiwe kupitia rushwa au ufisadi,” alisema Kificho.
Kificho ambaye alikuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalum la Katiba (BMK), alisema tamaa zimekuwa kubwa kuliko dhamana aliyopewa mtu katika utumishi wa umma ndiyo maana wanatanguliza maslahi yao kwanza.
“Kutokana na hali hiyo, mara nyingi hata unachotaka ukipate wengi hawakifanyii kazi vizuri, umepewa fedha ya rushwa, lakini bado hutimizi wajibu…tunahitaji kutoa elimu na kukumbushana katika kukabiliana na rushwa na ufisadi kwa kuwaeleza unapopewa dhamana unakuwa na jukumu na wajibu wa kutekeleza ipasavyo na utakachokipata ni matokeo ya utekelezaji wa dhamana husika,” alisema.
CCM NA MAKUNDI
Alisema hakuwahi kutoa fedha wakati wa uchaguzi kwa kuwa aliongoza jimbo la Makunduchi wakati wa chama kimoja, lakini kwa sasa utoaji wa rushwa unatokana na wanaoomba uongozi na jamii inayohusika kuchagua kiongozi.
“Hii ni sawa na kununu uongozi, hii inavuruga ‘commitment’ (kujitolea) ya mtu katika utendaji wake, anajitahidi alichotumia atumie njia mbalimbali katika kukirejesha kwa kutumia nafasi aliyopata kwa kijitizama yeye kuliko anaowaongoza,” anasema na kuongeza:
“Kuna hatari ya kupata baadhi ya viongozi ambao kwa muda wote watajiangalia wao bila kuangalia jukumu lake kwa wananchi.”
Kificho ambaye amewahi kuwa hakimu wa Mahakama ya Wilaya Pemba, alisema chama chochote kikijenga tofauti na kuwa na makundi ni lazima kitetereke, akaasa umuhimu wa kuwa na umoja na ushirikiano.
“Hali na mwenendo wa suala uliopo ambao hauna mwelekeo wa kuhudumia jamii ipasavyo siyo ishara nzuri kwa chama changu (CCM), wakati huu ndiyo wakati umoja na ushirikiano unahitajika zaidi ndani ya chama kuliko wakati wowote ili kuwa na uongopzi bora wa nchi,” alisema.
UTAWALA BORA NA MARAIS WALIOPITA
Alisema nchi zilizoendelea zilianza na utawala wa kiimla na kimabavu na baadaye kufikia utawala bora, hivyo Tanzania haiko katika hatua mbaya.
Kwa mujibu wa Kificho, wakati wa Sheikh Abeid Amani Karume, maendeleo yalikuja kwa muda mfupi, uchumi wa Zanzibar ulikuwa vizuri kuliko vipindi vingine vya uongozi na kwamba sababu zipo za ndani na nje.
“Kila wakati na kitabu chake, mfano suala la haki ya kujieleza au haki ya kusema, haikuwa rahisi wakati wa utawala wa marais waliopita kumsema Mwalimu Julius Nyerere wazi wazi, ila wapo ambao walikuwa wanaweza kumsema wazi wazi…kulikuwa na Mzee Mtandika (Masoud) aliweza kuzungumza na Mwalimu jambo lolote na hilo hilo ambalo aliweza kusema wengine hawawezi kusema,” alisema.
Alisema Mzee Karume aliweza kwenda Ikulu na kuongea na Nyerere jambo lolote, lakini hiyo ilitokana na wakati na mazoea ya mtu na mtu.Kwa maana hiyo, alisema unaweza kusifia wakati wa uongozi wa fulani kuliko wakati mwingine.
Alisema utawala bora na demokrasia vinakwenda sambamba, huku akikumbusha kuwa wakati wa Sheikh Karume hakukuwa na Baraza la Wawakilishi na Aboud Jumbe alirithi utawala kuanzia 1972 hadi 1984, lilianzishwa na kuwa na upanuzi wa demokrasia kidogo na kukua kwa utawala bora.
Kificho alisema wakati huo viongozi wengi wa Baraza la Wawakilishi walikuwa wa kuteuliwa kutoka kamati mbalimbali za Mapinduzi na hakukuwa na uchaguzi rasmi na baada ya Katiba kurekebishwa miaka ya 1984 yalianzishwa majimbo, hivyo wajumbe kuchaguliwa kutokana na viti maalum kama wanawake, vijana na washirika.
Alisema mwaka 1984 Ali Hassan Mwinyi alichukua urais wa muda wa Zanzibar ambako biashara ilikua kutokana na ruksa iliyokuwepo.“Kuweka sheria, taratibu na kanuni nyingi siyo utawala bora bali utazaa rushwa kwa kuwa katika kuziba kila mwanya ndiyo mwanzo wa kuwa na rushwa,” alisema.
Alisema Idrisa Abdul Wakil alikuwa muadilifu, hakupenda mivutano na alichukia uonevu alimtaja kuwa kiongozi wa kwanza kuvunja Baraza la Mapinduzi na kuanza upya na ndicho kipindi ambacho Maalim Seif Sharif Hamad alitolewa katika nafasi ya Waziri Kiongozi.
“Wengine waliondoa baadhi ya watu na kumuweka mwingine, lakini huyo alivunja lote na kuanza upya, demokrasia inabadilika, lakini utalawa bora unakua hatua kwa hatua kufuatana na wakati, siyo rahisi kusema au kulinganisha sasa ni bora kuliko zamani,” alisema.
Kificho ambaye amekuwa Spika tangu mwaka 1995, alikosoa utawala bora katika manunuzi ya serikali kwa kuwa umeruhusu mianya ya rushwa na bidhaa kununuliwa kwa bei kubwa.
“Mtiririko wa manunuzi una rushwa tele ndani yake, kupitia utaratibu uliopo unajikuta unanunua bidhaa bei kubwa, pamoja na uwazi uliopo consumer (mlaji) anaumia zaidi kuliko ambavyo angekwenda moja kwa moja kununua,” alisema na kuongeza:
“Demokrasia inafanya maendeleo kwenda taratibu na ndiyo maana wakati wa Mzee Karume kumekuwa na maendeleo ya haraka kwa kipindi kifupi kuliko wakati mwingine kwa kuwa aliweza kuamua na jambo likafanyika.”
UKUAJI WA UCHUMI
Alisema tatizo kubwa watu wanashindwa kufanya tathmini kujua tulipotoka, tulipo na tunakwenda wapi kwani ndiyo njia pakee ya kujua. Alisisitiza kuwa siyo kweli kudai uchumi wa Zanzibar unazidi kudidimia.
Alisema zamani miaka 30 au 40 kijana mdogo kuwa na nyumba nzuri haikuwa rahisi na hawakuweza kumiliki gari, lakini kwa sasa ni jambo la kawaida. Alieleza kwamba yote ni matokeo ya ukuaji wa uchumi.
Alitaja changamoto za sasa kuwa ni upatikanaji wa chakula cha siku hali ambayo ilikuwapo tangu zamani.“Kiwango cha maisha kimebadilika ukilinganisha na zamani, mahitaji yamekuwa mengi, mambo yaliyoonekana muhimu huko nyuma sasa yamekuwa mengi zaidi, miaka 20 nyuma maeneo mengi ya Zanzibar yalikuwa misitu, ila kwa sasa kuna nyumba nzuri ikiwa ni dalili ya ukuaji wa uchumi,” alifafanua.
“Zanzibar tuna upungufu wa rasilimali, rasilimali yetu ya asili ni mazao ya kilimo mbadala au nyongeza yake hakuna, kwa life standard (kiwango cha maisha) tulichofikia tunahitaji mapato mengine kuendelea ambayo ni bahari, lakini bado hatujaweza kuingia Bahari kuu, ila utafiti wa mafuta bado haujatoa matokeo kutueleza kama mafuta yaliyopo yanafaa kwa biashara,” alifafanua.
Alisema vyanzo vya mapato kwa Zanzibar ni vichache sana kwa kuwa wanategemea mazao ya kilimo ambayo yamekubwa na ufinyu wa ardhi, huku utalii ukikumbwa na changamoto za matukio ya ugaidi na vurugu wakati wa uchaguzi.
“Maeneo ya kutoka Fuoni mpaka Njia Kuu hadi Donge ni maeneo ya Kilimo ikiwamo kilimo cha karafuu ,lakini kwa sasa yamekuwa ni makazi na zao kuu ya biashara la karafuu limeshindwa kustawishwa ipasavyo, tunatafuta vyanzo vingine kwa ajili ya uchumi,” alisema.Kificho alisema upande wa Pemba ndiko kunalimwa karafuu kutokana na uwapo wa milima na mabonde na eneo lingine ni Micheweni.
CHANGAMOTO ZA UTALII
Alisema utalii siyo biashara ya kutegemea sana kwa kuwa inatetereka kwa urahisi na kwamba Zanzibar inatafuta vyanzo vingine vya mapato ili kuimarisha uchumi wake baada ya kilimo kukosa maeneo.
SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA
Alisema lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) lilikuwa ni kupunguza mivutano isiyo ya msingi ili kujenga ushirikiano baina ya wananchi kwani muda na fedha nyingi zilitumika kuondoa mivutano na kupambana na hujuma mbalimbali kuliko kutumikia wananchi.
“Ni afadhali kuijenga jamii ya watu wanaoshirikiana na kuifanya kazi kwa manufaa ya jamii, lakini itikadi zetu za kivyama zinatufanya kusiwe na kuaminiana kwa kuingiza itikadi na mitizamo ndani ya serikali kwa kila mmoja kuona akifanya hivi na vile ndipo atafanikiwa kushika hatamu ya dola, wakati hayo yanafanyika hayapaswi kuingilia madhumuni ya kuhudumia wananchi,” alifafanua.
UFANISI WA BARAZA LA WAWAKILISHI
Alisema Baraza la Wawakilishi kwa sasa haliaminiani kutokana na kila mmoja kuwa na itikadi ya chama, lakini siyo jambo kubwa sana kwa kuwa hailingani na wakati wa serikali moja ambayo kulikuwa na mivutano ya wazi.
“Inafika mahali tunajiuliza ni halali kutumia fedha za walipa kodi kutukana? Hata hivyo, ukiondoa tofauti za kutoaminiana, Baraza kwa sasa linafanya vizuri kuliko miaka ya nyuma,” alisema.
Alisema kwa sasa changamoto kubwa ya uendeshaji wa Baraza la Wawakilishi ni kutoaminiana kwa uwazi baina ya vyama vya CCM na CUF na kwamba unaathiri ufanisi wa chombo hicho.
Alisema kwamba viongozi wa vyama wana nafasi kubwa ya kukuza au kulimaliza suala hilo ili chombo hicho kitekeleze majukumu yake ipasavyo.Imeandikwa na Salome Kitomari, Raphael Kibiriti na Rahma Suleiman.
*Usikose habari kujua Kificho ni nani hasa ndani ya NIPASHE kesho.
CHANZO: NIPASHE