STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03 Disemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa amekuwa akitekeleza kikamilifu matakwa ya Katiba katika kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
Amesema kwa kuwa anaelewa vyema wajibu wake wa kuzingatia Katiba katika kutekeleza majukumu yake ya urais halazimiki kujibu shutuma au maneno ya kuukosoa uongozi wake kwa vile watu wanaofanya hivyo wenyewe hawaijui Katiba.
Dk. Shein ameeleza hayo leo wakati akizungumza na viongozi wa mashina na wenyeviti wa maskani za Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni siku yake ya tatu ya ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba kuimarisha Chama cha Mapinduzi.
“wakati nikitekeleza majukumu yangu ya kikatiba mimi sisikilizi maneno yao na wala siwajibu kwa kuwa wao wenyewe hawaifahamu Katiba iliyonipa mamlaka hayo” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa hata wengine wanapotosha jina la serikali.
Alifafanua kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa ndio jina rasmi wala si vinginevyo.
Kwa hivyo aliwahimiza wananchi kusoma na kuielewa vyema Katiba ya nchi kwa kuwa ndio sheria mama na kukosa kuifahamu hakumuondoshei adhabu mwananchi anapovunja katiba hiyo.
Katika mnasaba huo Dk. Shein alieleza kuwa wana CCM wana kila sababu za kujiv
unia na kujipongeza kwa kutekeleza Ilani yao ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa na kuwahimiza kuwaeleza wananchi juu ya mafanikio hayo.Alibainisha kuwa wako waliobeza baadhi ya ahadi za Serikali kama vile kujenga barabara ya kutoka Ole hadi Kengeja ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Serikali na Jumuiya ya Nchi Zinazotoa Mafuta kwa Wingi Ulimwenguni (OPEC).
“Naungana na maelezo yenu ya kuunga mkono utekelezaji wa Ilani yetu ingawa baadhi zimechelewa kwa sababu mbalimbali lakini utekelezaji huo utaendelea katika kipindi kilichobaki” Dk. Shein alieleza na kuwaambia viongozi hao kuwa ahadi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi zimeandaliwa kwa umakini mkubwa na kuangalia vipaumbele vya nchi.
Ndio maana alieleza kuwa kila baada ya miezi mitatu serikali inakutana kutathmini utekelezaji wa mipango ya serikali ambayo imezingatia Ilani ya CCM, Malengo ya Milenia na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini-MKUZA II.
Dk. Shein ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwaeleza viongozi hao kuwa katika Ilani yake ya uchaguzi CCM ilieleza kuwa haitabinafsisha biashara ya zao la karafuu tofauti na wapinzani badala yake itaimarisha zao hilo.
Aliongeza kuwa ndio maana Serikali ilichukua hatua madhubuti kulihami zoa hilo ikiwemo kupandisha bei ya karafuu na kuahidi kutoshusha bei hiyo hata pale bei ya zao hilo inaposhuka katika masoko ya dunia.
Kufuatia utekelezaji huo wa Ilani, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa hakuna wa kuizuia CCM kushinda uchaguzi mwaka 2015 na kusisitiza kuwa kinachotakiwa ni viongozi wa mashina na maskani kuunganisha nguvu na kuongeza kasi ya kuimarisha chama chao.
Katika risala yao kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, viongozi hao walieleza kuridhishwa kwao na namna anavyoongoza serikali iliyo chini ya mfumo wa umoja wa kitaifa pamoja na kusimamia vyema rasilimali za nchi.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kusimama kidete kupigania amani na utulivu Zanzibar pale zilipojitokeza dalili za uvunjifu wa amani kwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana nazo.
Kuhusu Katiba iliyopendekezwa, Vuai alifafanua kuwa makundi mengi yanayoipinga Katiba hiyo kwa maslahi binafsi wala sio kutetea maslahi ya mwananchi wa kawaida. Aliyataja baadhi ya makundi hayo kuwa ni pamoja na UKAWA unaojumuisha baadhi ya vyama vya siasa na watu wanaojiita kamati ya maridhiano.
Kamati hiyo ya maridhiano alieleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa haina uhusiano wowote na Chama cha Mapinduzi kama baadhi ya wajumbe wake wanavyojinasibu kuwa wanakiwakilisha katika kamati hiyo.
“watu hawa hawana mnasaba wowote na Chama cha Mapinduzi, hao wanajiita ama wanaodai kuwakilisha CCM mbona hawana barua ya uteuzi kama CCM inavyofanya katika kuteua wawakilishi wake” Vuai aliwaeleza viongozi hao wa mashina.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822