STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03 Disemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezitaka Wizara, Idara na taasisi za serikali kuhakikisha kuwa zinazifanyia kazi kasoro zinazogunduliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kasoro hizo zisiweze kujirudia tena.
Akizungumza mara baada ya kuzindua jengo jipya la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali huko Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba jana, Dk. Shein alisema kuzifanyia marekebisho kasoro zinazogunduliwa wakati wa ukaguzi kutaliwezesha Taifa kudhibiti na kuongeza ufanisi katika matumizi ya fedha na mali za umma.
Kwa hivyo amezihimiza tena Wizara na Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa zinatuma kwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kumbukumbu zote za hesabu na matumizi ya fedha kwa wakati uliopangwa ili Ofisi hiyo iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein ameupongeza uongozi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa upangaji mzuri wa mipango ya Ofisi hiyo unaozingatia matumizi mazuri ya rasilimali na upangaji wa vipaumbele.
“Juhudi zenu za kujenga ofisi mpya ni mfano mzuri wa kuigwa na Wizara na Taasisi nyingine za Serikali…hongereni kwa kuongoza kwa mfano hasa tukizingatia kuwa ujenzi huu wa majengo haya pamoja na vitendea kazi vya kisasa umegharimiwa na Serikali kwa asilimia mia” Dk. Shein alisema.
Alisema amevutiwa na uongozi wa ofisi hiyo wa kuweka kipaumbele katika kuimarisha mazingira ya kazi ambapo upatikanaji wa ofisi pamoja na vitendeakazi vya kisasa ndio vitu vilivyopewa uzito katika mipango yake huku masuala ya maslahi ya wafanyakazi yakifuatia baadae.
Kwa hivyo aliihakikishia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa Serikali itaendelea na jitihada zake za kuimarisha Ofisi hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa hatimae iweze kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya taifa.
“Serikali itahakikisha kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali inapewa nyenzo zote inazohitajika kutekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa” Dk. Shein alifafanua.
Katika mnasaba huo Mhe Rais aliwakumbusha wageni na wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa juhudi hizo za kuimarisha ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya serikali ya kuimarisha demokrasi na utawala bora kama ilivyoagizwa katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Tawala CCM ya mwaka 2010.
Akizungumzia kuhusu ushirikiano na washirika wa maendeleo, Dk. Shein aliikumbusha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa ina mchango mkubwa katika kuimarisha mashirikiano hayo kwa kusimamia vyema misaada inayopatiwa Zanzibar ikiwemo fedha kama mikopo na mingineyo na washirika hao ili kuzidisha imani yao kwa nchi.
Aliitaka Ofisi hiyo kuelewa kuwa hivi sasa suala la udhibiti na usimamizi mzuri wa fedha na matumizi ya rasilimali nyingine za nchi umekuwa “kigezo kikuu cha kuimarisha au kukatisha mashirikiano na washirika wa maendeleo likiwemo suala la upatikanaji wa misaada ya maendeleo”.
Dk. Shein aliieleza hadhara iliyohudhuria hafla hiyo kuwa ni jambo la kutia moyo na faraja kwa Serikali na wananchi kuona kuwa washirika wa maendeleo wamekuwa wakieleza kuridhika kwao na namna serikali inavyoimarisha utawala bora na inavyotumia rasilimali zake.
Sambamba na uzinduzi wa jengo hilo, Dk. Shein alizindua pia kitabu cha historia ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambacho kimeandikwa kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi huko viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa SUZA, Kampasi ya Beit El Raas, Unguja, tarehe 03 Januari mwaka huu.
Wakati huo huo, akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alimhakikishia Mheshimiwa Rais na wageni waalikwa kuwa watumishi wa Ofisi hiyo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa wajibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Dk. Mwinyihaji aliishukuru serikali kwa kuunga mkono jitihada za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kutekeleza majukumu yake jambo ambalo limewezesha Ofisi hiyo kupata mafanikio makubwa na hivyo kuchangia jitihada za serikali za kuimarisha utawala bora.
Kwa upande wake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bibi Fatma Mohamed Said alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Maalum wa Miaka Kumi wa Kuimarisha Ofisi hiyo ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na tekinolojia na kukidhi viwango vya kiukaguzi vilivyowekwa kitaifa na kimataifa.
Moja ya lengo la mpango huo alifafanua ilikuwa ni kujenga majengo mapya na kuhama katika majengo ya zamani na mengine ya kukodi pamoja na kuweka vifaa vipya hivyo uzinduzi wa jengo hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa lengo hilo.
Bibi Fatma alibainisha kuwa chini ya mpango huo Ofisi yake imeweza kuwaendeleza kimafunzo watumishi wake hadi kupandisha kiwango cha wataalamu kutoka asilimia kumi mwaka 2004 hadi asilimia tisini mwaka 2014 na kutolea mfano mtumishi aliyeajiriwa akiwa na elimu ya kidato cha nne ambaye sasa yuko masomoni anachukua shahada ya uzamivu.
Matokeo ya mpango huo alisema yameifanya Ofisi hiyo kufanyakazi zake kwa ufanisi na kubainisha kuwa hata mfumo na vifaa vya tekinolojia ya habari na mawasiliano katika ofisi zake zote vikiwemo vya jengo lililofunguliwa vimewekwa na watumishi wa ofisi hiyo na kusisitiza kuwa ofisi yake “imejipanga vizuri kuelekea katika mfumo wa E-government”.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa kuongeza maslahi ya watumishi wa ofisi yake na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ziliyowekwa.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822