Na Salum Vuai, Maelezo
JUMUIYA ya Wazanzibari wanaoishi nchini Canada (ZANCADA), imetoa msaada wa sare za wauguzi kwa ajili ya hospitali za Zanzibar, kwa lengo la kupunguza tatizo la uhaba wa sare hizo.
ZANCADA imekabidhi jozi 300 za sare hizo zenye thamani ya shilingi milioni kumi, kwa Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya juzi ofisini kwake Mnazimmoja.
Hatua hiyo ni kuitikia wito wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kuwataka Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), kuisaidia nchi yao katika jitihada zake za kuleta maendeleo.
Mmoja wa viongozi wa jumuiya hiyo yenye makao makuu yake jijini Toronto Bishara Abdalla Mansour, amesema ZANCADA imekuwa na utamaduni wa kuwakumbuka ndugu zao wenye mahitaji popote walipo duniani.
Amesema kupitia utaratibu huo, jumuiya yao itaendelea kutoa misaada ya hali na mali kila mahitaji yatapojitokeza.
Naye Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya, akitoa shukurani kwa niaba ya wizara yake na serikali, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka, kwani uhaba wa sare ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wauguzi na madakatari wengi nchini.
Alisema ingawa ni wajibu wa wizara kuwapatia sare wafanyakazi wake, lakini mara nyingi inakwazwa na ufinyu wa bajeti.
Aliwaomba wana Diaspora hao kuendelea na moyo wa kuikumbuka nchi yao ambayo inafanya jitihada kubwa za kustawisha maisha ya wananchi wake.
Aidha alitaka misaada kama hiyo iwalenge zaidi wafanyakazi wa vijiini ambao alisema ndio wanaokabiliwa na changamoto kubwa zaidi ya wale walioko mjini.
Dk. Sira pia aliwakumbusha Wazanzibari wote wanaoishi nje ya nchi, kuhakikisha wanalinda heshima ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla, kwa kutojihusisha na mambo maovu yanayoweza kulipaka matope taifa lao.
“Mkiwa nje msijisahau mkaacha kufanya lililowapeleka huko ambalo ni kutafuta maisha kwa manufaa yenu, familia na nchi, na kujiingiza katika vitendo vitakavyoleta taswira mbaya kwa taifa”, alisisitiza.
Nao wana jumuiya hiyo Zamil Rashid, na Al Amin Ahmed, Suleiman Al Riyami na Rashid Omar Ghassany, waliahidi kuendelea kushikamana na kuisaidia nchi yao, kwani ndiyo iliyowasomesha na kuwalea.