Na Fatuma Kitima,DAR ES SALAAM
Kampuni ya Global Education Link (GEL) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),Wizara ya Elimu na Ufundi pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) wameandaa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya elimu (TIEE) yanayotarajiwa kufanyika Disemba 10 hadi 14 mwaka huu katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Global link Education,Abdulmalik Mollel, alisema lengo la maonyesho hayo ni kutambulisha wadau wa elimu kwa pamoja ili kuweza kutoa huduma ya pamoja kwa wananchi na kuwaelimisha juu ya mambo muhimu yaliyopo katika kila sekta.
Alisema ushiriki wa asasi mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi utakuwa na chachu ya mabadiliko ya elimu kwa kupitia mpango wa matokeo makubwa sasa.
Aidha alisema maonyesho hayo yataleta manufaa makubwa na changamoto chanya hasa katika kuongeza ushindani katika sekta ya elimu ambayo itasaidia mpango wa matokeo makubwa sasa.
Maonesho hayo yanatarajiwa kupata washiriki zaidi ya 500 na wananchi mbalimbali zaidi ya 350,000 kutoka ndani na nje ya nch.
Kauli mbiu ya maonesho hayo ni ‘kuweka jitihada za pamoja katika kuboresha mfumo wa elimu Tanzania ni njia thabiti ya kuleta maendeleo endelevu katika taifa.’