Na Ameir Khalid
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdilahi Jihad Hassan, amesema shughuli za uvuvi zinapaswa kusimamiwa vyema, ili vizazi vijavyo viweze kurithi rasilimali nzuri zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Alitoa kauli hiyo katika ukumbi ya hoteli ya Grand Palace Malindi, alipokuwa akizindua mpango mkakati wa utawala na usimamizi wa shughuli za uvuvi Zanzibar, ukiwa na lengo la kuwa na uvuvi endelevu.
Alisema shughuli za uvuvi zinapaswa kusimamiwa vyema ikiwa ni mpango ambao utasaidia kuwa na lengo na nia ya matumizi mazuri na endelevu ya bahari ili wavuvi na wananchi wa Zanzibar waweze kunufaika na rasilimali ya bahari iliyopo.
Alisema katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa ni vyema kuimarishwa mfumo wa utawala na usimamizi wa kuwawezesha wavuvi wa kienyeji kuvua samaki katika bahari kuu.
Mapema Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Kassim Gharib Juma, alisema sekta ya uvuvi Zanzibar inachangia kwa asilimia 7.1 katika uchumi wa Zanzibar, huku ikibainika kuwa asilimia kubwa ya wavuvi wa Zanzibar wanatumia uvuvi wa kienyeji.
Alisema mipango inayofanywa ni kuhakikisha kunapatikana mafanikio makubwa ya uvuvi ifikapo mwaka 2020 malengo yote yaliokusudiwa tayari yawe yametekelezwa