Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein: Wanaoipinga Katiba pendekezwa wanatetea maslahi yao binafsi

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                        05 Disemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
Wananchi wametakiwa kuwa makini na watu wanaoipinga Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba kwa madai kuwa wanatetea maslahi ya Zanzibar wakati wanafanya hivyo kutetea maslahi yao binafsi.
 
Akizungumza na viongozi wa mashina na wenyeviti wa maskani za Chama cha Mapinduzi wa wilaya ya Mkoani jana, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alibainisha kuwa watu hao wanawadanganya wananchi na ndio maana wanapoipinga Katiba hiyo wanashindwa hata kunuu vifungu vya Katiba kutetea hoja zao.
 
“Msikubali kudanganywa na mtu ye yote kuhusu suala hilo (akiimanisha ardhi). Hawa watu wanafanya ujanjaujanja tu ndio maana wanashindwa kunuu vifungu vya Katiba vinavyosema hayo wayasemayo” Dk. Shein alieleza.
 
Aliwahakikishia wananchi kuwa suala la ardhi katika Katiba iliyopendekezwa liko wazi na kwamba kwa Zanzibar ardhi inabaki kuwa mali ya serikali na ndio itakayoamua matumizi yake.
 
Katika mnasaba huo aliwataka wana CCM na wananchi wa Zanzibar kuisoma Katiba iliyopendekezwa na kuelimishana kadri wanavyoweza huku wakikabiliana na watu wanaoipinga kifungu kwa kifungu si kwa maneno matupu kama wanavyofanya watu hao.
 
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kuongeza kasi ya kuimarisha chama chao huku akisisitiza uzingatiaji wa Katiba ya chama hicho katika uendeshaji wa shughuli zake.
 
Alibainisha kuwa Chama cha Mapinduzi kuendelea kuwa namba wani (moja) ni pamoja na kufuata Katiba na kanuni zake na ndio maana wapinzani wake wanakiogopa kwa kuwa wanaelewa uwezo na uzoefu wake katika kuendesha siasa nchini.
 
Katika mkutano huo viongozi mbali mbali walitoa maoni na mapendekezo pamoja na baadhi ya changamoto za kimaendeleo zinazoyakabili maeneo yao ambapo Dk. Shein alizipokea na kuahidi kuzifanyia kazi na kwa kuzielekeza katika wizara husika kuzitafutia ufumbuzi.
 
Wakati huo huo viongozi wa Chama Mapinduzi wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba wameahidi kushirikiana na viongozi wapya wa Mkoa na Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
 
Katika risala yao kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, viongozi hao walipongeza na kuunga mkono uteuzi huo wa Mkuu wa Mkoa na Wilaya na pia kumshukuru Rais kwa uongozi wake madhubuti unaozingatia Katiba na Sheria hivyo kuiweka nchi katika hali ya utulivu na amani.
 
Ziara za kuzungumza na viongozi hao wa wilaya zote za Chama cha Mapinduzi zilianza kiswani Unguja tarehe 27 Novemba, 2014 na kumalizika jana ambapo kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai jumla ya viongozi 11,961 walihudhuria mikutano hiyo na viongozi wa maskani walikuwa 794.
 
Alifafanua kuwa kati ya viongozi hao, 121 walipata fursa ya kuchangia mikutano hiyo kwa kutoa mawazo, kuuliza maswali na kutoa mapendekezo yao mbele ya Rais.
 
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa mikutano hiyo imeonesha uimara wa chama hicho na kwamba kiko tayari kwa uchaguzi ujao na kushinda kwa kishindo.
 
“mabalozi 11,961 na viongiozi wa maskani 794 hili ni jeshi kubwa ambalo litaongoza kupitisha Katiba iliyopendekezwa pamoja na kuiwezesha CCM kushinda uchaguzi mwaka 2015 kwa kishindo” Ndugu Vuai alieleza.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                               

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles