Na Edna Bondo
MAISHA tunayoishi yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo baadhi yake zimeweza kutatuliwa, lakini zingine zinashindakana hadi pale jamii inapopata msaada kutoka nje.
Hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kutokana na hali halisi ya maisha tunayoishi kuwa na mifumo inayoifanya jamii kushindwa.
Kutokana na mifumo na hali ngumu ya maisha inayoifanya jamii kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu, wakati mwingine serikali hukiri kushindwa hivyo kuhitaji msaada kutoka katika sekta binafsi.
Misaada hiyo ambayo imezaa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi katika kusaidia miradi inayosaidia jamii (PPP) imekuwa ikifanywa na kampuni mbalimbali, taasisi zisizo za kiserikali kama vile makanisa,misikiti pamoja na benki, jambo ambalo limeonekana kuleta matokeo chanya.
Aidha, matokeo hayo chanya chini ya mpango wa PPP kwa asilimia kubwa yameweza kutimiza malengo ya milenia.
Chini ya mpango wa PPP, sekta ya benki nchini imekuwa ikizidi kupanuka siku hadi siku kutokana na kuelekeza sehemu ya faida yake katika kuisaidia jamii.
Mbali ya kuwa na umuhimu katika jamii zetu, lakini pia taasisi hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo.
Aidha, taasisi hizo zimekuwa msaada mkubwa katika kusaidia jamii katika huduma mbalimbali hususan elimu, afya pamoja na kuwawezesha wajasiriamali wadogo.
Mwanzoni wa wiki hii, Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ), iliendesha semina ya siku moja jijini Dar es salaam iliyokuwa ikielezea shughuli za benki ya kiislamu (Islamic Banking) kwa wadau wake sambamba.
Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli ni miongoni mwa wadau wa benki hiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi ambapo katika hotuba yake amesifu juhudi zinazofanywa na benki hiyo ikiwemo ukuaji wake ulioleta matokeo chanya.
Anasema PBZ inastahili pongezi tangu kutokana na ukuaji wake wa asilimia 2 pamoja na kuongezeka kwa amana zake hadi kufikia sh. bilioni 72,
Anasema ukuaji huo umeweza kuwa msaada mkubwa kwa wajasriamali wadogo pamoja na huduma mbalimbali za kijamii, jambo ambalo limeipunguzia serikali mzigo kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na PBZ kuwa sehemu ya msaada mkubwa katika Jamii ya Watanzania bara na visiwani, Gavana Reli anasema BoT itahakikisha inaweka miongozo na mazingira mazuri yatakayorahisisha shughuli zote za Benki ya kiislamu Tanzania, ili kuepuka athari zozote za fedha, ili kuisaidia benki hiyo izidi kukua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Juma Amour, anasema anajivunia mafanikio ya benki yake kwa sababu mbali ya yale yaliyotajwa na Gavana Reli, lakini pia wameweza kufungua matawi manne.
Anasema kwa kipindi cha miezi miwili ijayo, benki hiyo itafungua matawi mengine katika mikoa ya Dar es salaam na Mtwara, ili kupanua wigo wa huduma kwa jamii.
Pamoja na hayo, anaahidi benki hiyo kuendelea kushirikiana na kusaidia mambo mbalimbali, ili kuhakikisha ustawi wa maendeleo ya jamii si tu visiwani Zanzibar, lakini pia bali Tanzania nzima kulingana na faida itakayopatikana.
“Mafanikio mengine ambayo ninaweza kujivunia juu PBZ ni kwamba tumeweza kuvuna wateja zaidi ya 45,000 pamoja na kusaidia jamii katika mambo mbalimbali ikiwemo vituo vya watoto yatima.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwahamasisha watanzana kufungua akaunti zao katika benki yetu,”anasema Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia kuhusu changamoto, anasema kubwa linalowakabili ni kukosekana kwa ufahamu kwa wateja juu ya benki za kiislamu ambazo zinaongozwa na shariah, hivyo kwa upande wao wanajitahidi kutoa elimu, ili kujenga uelewa.
Historia ya PBZ
Benki ya Watu wa Zanzibar (IslamicBanking section) ilianzishwa na maamuzi ya bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo mwaka 2007 baada ya kufanyika utafiti ambao ulibaini kuwa wananchi wengi hawaweki fedha zao benki kutokana na imani za kidini
ambazo zinakataza riba.
Anasema benki hiyo ilianza kutoa huduma zake rasmi mwaka mwaka 2011 na kwamba dira na dhamira ya PBZ ni kutoa huduma kwa kufuata misingi ya sharia, kusaidia serikali katika kukuza uchumi, ustawi wa jamii na kupunguza umasikini.
Pia anasema PBZ inatoa huduma kwa jamii kwa kufuata maadili ya haki, uadilifu kuwajibika katika kutunza amana katika misingi ya kitaalamu, lakini pia ina huduma ambazo zinawazesha wateja wake kufungua akaunti mbalimbali.
Chanzo : Tanzania Daima