Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Ofisa wa Kampuni ya Mitandao ta Teknolojia ya Mawasiliano ya Vietnam Tawi la Dar es salaam Bibi Le Duy Duong Ofisini kwake Vuga.Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi naTeknolojia ya SMT Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa Viettel Tanzania Bwana Nguyen Thanh Quang.
Balozi Seif akizunguimza na Ujumbe wa Kampuni ya Mitandao ta Teknolojia ya Mawasiliano ya Vietnam Tawi la Dar es salaam ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Viettel Tanzania Bwana Nguyen Thanh Quang mara baada ya mazunguimzo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Viettel Tanzania Bwana Nguyen Thanh Quang mara baada ya mazunguimzo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Bodi Mpya ya Mpango wa kurasimisha rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania { MKURABITA } ofisini kwake Vuga.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mh. John Chiligati ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mkoani Singida.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Uongozi wa Kampuni ya Uwekezaji wa Mtandao wa Mawasiliano ya Teknolojia ya kisasa ya Vietnam { Viettel Global Investment JSC. } umeonyesha nia ya kutaka kutoa huduma za mawasiliano kwa njia ya mtandao wa Kisasa katika maeneo ya Vijiji hapa Zanzibar.
Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Tawi la Tanzania Bwana Nguyen Thanh Quang akiuongoza ujumbe wa Viongozi watatu wa Kampuni hiyo alieleza hayo wakati akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Nguyen alisema kwamba Kampuni hiyo kwa kiasi kikubwa inaelewa umuhimu wa kizazi kipya kupatiwa elimu bora inayokwenda na wakati wa sasa wa Teknolojia ya mawasiliano ili kiwe na uwezo kamili wa kukabiliana na maisha yao ya baadaye.
Alisema hatua ya kutiliana saini mkataba na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya ujenzi wa Vituo vya huduma za mawasiliano ya mtandao katika maeneo ya vijiji visivyo na huduma hizo ni miongoni mwa malengo ya Kampuni hiyo.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Viettel Tanzania Limited alimueleza Balozi Seif kwamba Taasisi hiyo iko tayari kutoa huduma kama hizo kwa upande wa Zanzibar endapo watapata fursa ya kufanya hivyo katika mamlaka inayohusika.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d aliutaka Uongozi wa Kampuni hiyo kufanya utafiti wa kitaalamu katika kuangalia namna gani huduma zao za mawasiliano wanaweza kuzisambaza vijijini.
Waziri Aboud alisema katika kufanikisha azma hiyo aliutaka Uongozi wa Kampuni hiyo kufanya mawasiliano na wataalamu wa masuala ya teknolojia na mawasiliano hapa Zanzibar ili kuwa na mwanzo mzuri kwa Kampuni hiyo kuweza kutekeleza azma yake njema kwa mustakabala wa Jamii.
Mapema Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Makame Mnyaa Mbarawa alisema uwepo wa Kampuni hiyo Nchini Tanzania umekuja kufuatia ziara ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda Nchini Vietnam ambapo alitoa fursa kwa makampuni mbali mbali ya uwekezaji vitega uchumi kutumia fursa za Tanzania kuwekeza Nchini Tanzania.
Profesa Mbarawa alisema Kampuni hiyo tayari imeanza kuwekeza katika mradi wa mawasiliano Vijijini ambapo miongoni mwa makubaliano yake na Serikali imepanga kujenga vituo 4,000 vya mawasiliano kwenye maeneo ya vijiji vyenye ufinyu wa mawasiliano Nchini Tanzania.
Alisema mradi huo utakwenda sambamba na ujenzi wa mkongo wa mawasiliano ambapo Kampuni hiyo pia itatoa huduma za mitandao ya mawasiliano katika Hospitali za Wilaya, Ofisi za Halmashauri pamoja na ofisi za Polisi na Shule za Wilaya.
Akitoa shukrani zake kwa Uongozi wa Kampuni hiyo ya Viettel Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema bado mpaka sasa yapo baadhi ya maeneo vijijini yanakosa huduma za mawasiliano ya mitandao pamoja na simu.
Balozi Seif aliueleza Uongozi wa Kampuni hiyo ya Viettel Tanzania kwamba zipo taasisi za mitandao kwa kushirikiana na wataalamu waliojaribu kufanya utafiti wa kuenea kwa huduma hizo za mawasiliano na kugundua hitilafu hiyo.
Kampuni ya Viettel Global Investment JSC tayari imeshawekeza katika Mataifa ya Cambodia, Laos, Hait,. Msumbiji,Timor ya Mashariki,Peru, Cameroun Burundi na Tanzania katika masuala ya Teknolojia, Mawasilino pamoja na Teknolojia ya Habari.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana na Uongozi wa Bodi Mpya ya Mpango wa kurasimisha rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania { MKURABITA } iliyofika Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika dhamana hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mheshimiwa John Chiligati ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mkoani Singida alisema utafiti uliofanywa na Bodi hiyo kujua rasilmali ya Taifa umegundua kwamba asilimia 90% ya shughuli za Watanzania pamoja na asilimia 86% ya mali zao zimejificha zikifanywa nje ya utaratibu wa kisheria.
Mh. Chiligati alisema wataalamu wanapofanya majumuisho ya pato la Taifa inawawia vigumu kutokana na vyombo vya fedha kukosa uhusiano na sehemu hizo mbili.
Mwenyekiti huyo wa bodi ya Mkurabita alifahamisha kwamba mfumo wa urasilimishaji umelenga kutambuliwa kwa rasilimali za Taifa katika vyombo vinavyohusika pamoja na kuunganishwa na mtaji.
Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Ofisi ya msajili wa ardhi kwa kuanza kupima ardhi ambayo ndio rasilmali kuu ya Taifa jambo ambalo alieleza kwamba limepokewa vyema na wananchi walio wengi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mkurabita Bibi Serapia Mgeni alisema kwamba Maafisa wa Biashara wana wajibu wa kuelimisha na kuelekeza wafanyabiashara ndogo ndogo badala ya kuendelea na mpango wa kukamata wale wasio na vibali vya biashara.
Bibi Serapia alifahamisha kwamba Mpango wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge Tanzania { MKURABITA } umelenga kuzijengea uwezo Taasisi zilizojikubalisha kusaidia jamii katika masuala ya kuimarisha uchumi wa Taifa.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Bodi hiyo ya Mkurabita kwa kusimamia utekelezaji wa uimarishaji wa uchumi katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Balozi Seif alisema Uongozi wa Mkurabita una wajibu wa kuelimisha wananchi waelewe malengo ya chombo hicho yaliyojikita zaidi katika kusimamia uchumi wa taifa hasa kupitia wafanyabiashara wadogo wadogo.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikemea tabia ya baadhi ya watendaji wa taasisi na mashirika ya umma kuendeleza urasimu ambao umekuwa ukipigiwa kelele za kudhoofisha maendeleo ya Taifa.
Balozi Seif aliuahidi uongozi huo wa Bodi ya Mkurabita kwamba Serikali Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaangalia upya suala la usajili wa biashara ndogo ndogo wa Zanzibar ulingane na ule wa Tanzania Bara ili kutoa nafuu kwa wahusika.