Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Wabunge na Wawakilishi Wapunguzwe Bunge la Katiba. Wasema Katiba ni ya Wanasiasa.

$
0
0
Na Asya Hassan
SERIKALI imetakiwa kuivifanya marekebisho kifungu cha 22 (a) na (b) cha sheria ya mabadiliko ya katiba namba 8 ya 2011, kwa kuwa kimetoa mamlaka makubwa kwa Wawakilishi na Wabunge kufanya maamuzi kuhusu katiba mpya.

Vifungu hivyo kwa pamoja, vimetoa mamlaka kwa Wabunge na Wawakilishi wote kuwa wajumbe wa bunge la katiba.

Washiriki wa mjadala wa mchakato wa katiba mpya, walisema wana hofu huenda katiba itakayopatikana haitakuwa ya wananchi kwa kuwa wajumbe hao wataweka mbele zaidi maslahi ya vyama vyao.

Wakichangia mjadala huo uliofanyika ukumbi wa Eacrotanal Mjini Zanzibar jana, walisema wananchi wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi ya kuamua katiba waitakayo na si wanasiasa.

“Kama vifungu hivi havitaondolewa tunahofia katiba itakayopatikana haitaakisi matakwa ya wananchi wengi, badala yake itakuwa ya vyama vya siasa,” walisema.

Walisema katiba inayotarajiwa kupatikana ni ya wananchi na enzi za wanasiasa kufanya maamuzi zimepita.

Walisema wajumbe wa bunge la katiba lazima wapunguzwe ili kutoa nafasi kwa wananchi wa kawaida, wakulima, wafanyabiashara, wasomi, na asasi za kiraia ambao ndio waathirika wakubwa kushiriki kuamua katiba waitakayo na si kuchagulia katiba na watu wengine.

Nae Katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Yahya Khamis Hamad, alisema huu ni wakati pekee kwa wananchi kupata katiba waitakayo na kutahadharisha kwamba iwapo watafanya makosa wasitarajie fursa hiyo kuipata tena.

Alisema mchakato wa mabadiliko ya katiba umepata mafanikio na Watanzania wengine wameonesha kuipokea rasimu hiyo kwani mambo yaliyomo yanaonekana kukidhi haja.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakar alisema hiyo ni fursa muhimu kwa Watanzania kutoa maoni yao juu ya katiba wanayoitaka.

Aliwataka wachangie rasimu hiyo kwa maslahi ya nchi na vizazi vijavyo.

Mjadala huo wa siku moja umeandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>