HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL,
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIA
KATIKA UZINDUZI WA MAJENGO YA TAASISI YA MAFUNZO YA UANASHERIA KWA VITENDO TANZANIA
TAREHE 22 DESEMBA, 2014
Mhe. Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro (Mb)
Waziri wa Katiba na Sheria;
Mhe. Mohamed Chande Othman
Jaji Mkuu wa Tanzania ;
Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb)
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria;
Ndugu Maimuna K. Tarishi
Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria;
Ndg. George Masaju
Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Taasisi ya
Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ;
Ndg. Hussein Kattanga
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ;
Mhe. Said Mecky Sadick
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ;
Mhe. Jordan Rugimbana
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni;
Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika
Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria
kwa Vitendo Tanzania ;
Bi. Patricia McCullagh
Kiongozi wa Timu ya Wadau wa Maendeleo
katika Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria
(Legal Sector Working Group);
Wadau wa Maendeleo;
Watumishi na Wanafunzi wote wa Taasisi ya
Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa. Ninakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya uzinduzi wa majengo ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania . Mmenipa heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia muhimu ya Taasisi hii.
Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria;
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa wale wote walioshiriki kubuni wazo la kuwa na majengo na miundombinu ya aina hii na kufanikisha ujenzi wake. Juhudi zao na moyo wao wa kupenda maendeleo katika sekta ya sheria ndio umetufanya tujumuike hapa leo kushuhudia mafanikio haya. Hakika hili ni jambo la kujivunia. Vile vile, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Wajenzi na Mhandisi Mshauri kwa kazi nzuri waliyofanya ya ujenzi wa majengo na miundombinu hii. Sote tunayaona majengo yalivyojengwa vizuri na kwa ustadi mkubwa.
Kwa namna ya pekee, ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Wadau wa Maendeleo walioshiriki kupitia Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria nchini kuchangia ujenzi wa majengo haya. Wadau hawa ni pamoja na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Canada (DFATD) ambalo zamani lilijulikana kama (CIDA), Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Denmark (DANIDA) na Benki ya Dunia (World Bank). Ninatambua pia kuwa Programu hii imechangia maendeleo makubwa katika Sekta ya Sheria hususan katika ujenzi wa miundombinu ya taasisi mbalimbali zikiwemo Mahakama ya Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pamoja na mambo mengine, Programu hii imewezesha watumishi katika Sekta ya Sheria kujenga na kuimarisha uwezo wao wa kutoa huduma na imesaidia upatikanaji wa vitendea kazi na nyenzo mbalimbali kama vile samani na magari. Haya yote yamechangia katika kuiwezesha Sekta nzima ya Sheria kufikia dira yake ya Haki Sawa kwa Wote na kwa Wakati.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kuanzishwa kwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ni tukio la kihistoria katika Nchi yetu. Kabla ya kuanzishwa kwa Taasisi hii, mafunzo ya uanasheria kwa vitendo kwa wahitimu wa Shahada ya Kwanza ya Sheria ya vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi yalikuwa yanaendeshwa na kusimamiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali chini ya Programu iliyokuwa ikiitwa Internship.
Kuanzishwa kwa Taasisi hii ni matokeo ya mapendekezo ya Tume ya Msekwa ya 1977 (The Judicial System Review Commission) na Ripoti ya Bomani ya 1996 (The Legal Task Force Report) ambazo pamoja na mambo mengine, zilipendekeza kuanzishwa kwa chombo mahsusi cha kutoa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo. Mapendekezo haya yalitiwa nguvu na ongezeko la wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria na ongezeko la vyuo vinavyotoa shahada za Sheria nchini; na hivyo kuifanya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushindwa kumudu na kusimamia programu ya Internship.
Chini ya programu ya Internship wahitimu walikuwa wanamaliza wakiwa wamepata sifa za kuajiriwa katika utumishi wa umma na hawakuwa na sifa za kusajiliwa moja kwa moja kuwa mawakili wa kujitegemea na ililazimu wapitie utaratibu mwingine wa kufanya mitihani ya uwakili yaani “Bar Examinations”. Nimeambiwa kwamba wahitimu wa Taasisi hii wanatoka hapa wakiwa na sifa za kusajiliwa kuwa mawakili.
Pamoja na kutoa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo, nimeambiwa pia kwamba Taasisi hii kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika itakuwa inatoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo kumudu gharama za mawakili. Ni imani yangu kwamba huduma ya msaada wa kisheria itakayokuwa ikitolewa katika Taasisi hii itakuwa kichocheo kwa wananchi wengi wasio na uwezo, kufikia haki ambayo wamekuwa wakiitafuta.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nimefurahishwa kusikia kuwa ubora wa elimu ni jambo mnalolizingatia na kulipatia kipaumbele. Jambo hili ni muhimu sana kulisisitiza na kulizingatia kwani tunataka wahitimu wa Taasisi hii wafanane na mahitaji halisi ya huduma za kisheria zinazotakiwa. Wanapaswa kuwa na weledi katika sheria, wenye maadili na watu wasiotiliwa shaka katika kusimamia haki. Ningependa kuona wahitimu wa Taasisi hii wanathaminiwa katika soko la ajira na pia wanafungua fursa za ajira kwa wengine katika ofisi zao.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Ninapenda kuukumbusha uongozi na menejimenti ya Taasisi hii kuwa mnayo dhamana na wajibu mkubwa katika kutoa mafunzo bora kwa wahitimu wa Shahada ya Kwanza ya Sheria ili wawe mawakili wa kujitegemea au watumishi katika Taasisi za Umma. Kwa kuwa hii ni Taasisi ya aina ya pekee nchini kwetu, ni wajibu wenu kuhakikisha Taasisi hii inafanikiwa.
Changamoto iliyo mbele yenu ni kuthibitisha kuwa kuanzishwa kwa Taasisi hii ni bora kuliko utaratibu uliokuwepo awali. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuhakikisha kuwa mna mipango mizuri ya kujenga Taasisi yenye hadhi na ubora wa hali ya juu. Kazi hiyo ni kubwa, hivyo ni vyema mkaweka mikakati madhubuti na mipango thabiti ya utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini.
Aidha, jumuiya yote inao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, maarifa na weledi ili dhima ya Taasisi hii ya “Excellence in Legal Practice” iweze kutimizwa kwa ukamilifu. Timizeni wajibu wenu ipasavyo ili Taasisi hii iwe kivutio kwa wahitimu wa Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni imani yangu kuwa hili liko ndani ya uwezo wenu na mkiwa na dhamira ya dhati, linawezekana.
Ndugu Wanafunzi wa Taasisi;
Naomba wote muone fahari ya kuwa wanafunzi katika Taasisi hii. Nawasihi mjitume kwa kadri ya uwezo na vipaji mlivyopewa na Mwenyezi Mungu mfanikishe kile kilichowaleta hapa. Jifunzeni kwa bidii mfaulu vizuri ili mkihitimu muwe kielelezo kizuri cha mafanikio na ubora wa Taasisi hii. Taifa letu linawategemea nyie kama wataalam katika maeneo mbalimbali ya fani ya sheria.
Mheshimiwa Waziri;
Nimesikia changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili Taasisi tangu kuanzishwa kwake. Nawapongeza kwa dhati, Mheshimiwa Waziri na wenzako kwa ubunifu wenu na hatua mnazochukua katika kukabiliana na changamoto hizo. Nawaahidi ushirikiano wangu na wa serikali katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Pamoja na changamoto hizo, nitumie fursa hii kuwasihi kuyatunza majengo na miundombinu yote ya Taasisi ili iendelee kuwa katika hali nzuri. Hakikisheni pia mnatunza vizuri mazingira ya Taasisi hii ili yawe ya mfano kwa Taasisi zingine Wahenga walisema “Kitunze Kidumu”. Vile vile, nimeona jitihada mnazofanya za kupanda miti. Nawasihi muendelee na muongeze jitihada hizo kwa maeneo ambayo bado hamjafanya hivyo.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nimepata nafasi ya kutembelea miundombinu ya Taasisi hii na kwa namna ya pekee nimevutiwa na jinsi Mahakama ya Mafunzo itakavyokuwa inafanya kazi kupitia “Mock Trial” niliyoishuhudia hivi punde.Mahakama hii ya Mafunzo ina umuhimu mkubwa sana kwa wanafunzi wa Taasisi hii kwani itawawezesha kujifunza si tu kwa nadharia bali na kwa vitendo namna ya kuendesha mashauri mbalimbali na kupata uzoefu. Kwa mfano, kupitia video-link wanafunzi wa Taasisi watakaokuwa katika kumbi za kufundishia wataweza kuona moja kwa moja kinachoendelea katika Mahakama hiyo.
Mahakama hii ya Mafunzo ina vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia kurahisisha uendeshaji wa mashauri. Ningependa kuona kwamba Mahakama hii haitumiki tu kwa ajili ya mafunzo; bali inatumika kuendesha mashauri mbalimbali na iwe ni mfano wa uendeshaji wa mashauri kwa kutoa maamuzi ya haki na kwa wakati.
Naomba nimalizie hotuba yangu kwa kuwashukuru wananchi wanaoishi Sinza na maeneo mengine yanayoizunguka Taasisi kwa upendo, ujirani mwema na kwa kuishi vyema na wanajumuiya wa Taasisi hii. Nawaomba muendelee na moyo na ushirikiano huo. Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na mafanikio tele.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.