Na Husna Sheha
WANANCHI wa kijiji cha Makunduchi wametakiwa kuendeleza mshikamano na kujiepusha na migogoro ili kulibakisha eneo hilo kuanedelea kuwa kitovu na chemchem ya utulivu na elimu kama ilivyokuwa zamani.
Wito huo ulitolewa jana na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi, wakati akizungumza na baadhi ya wazee wa kijiji hicho katika ukumbi wa afya Makunduchi wilaya kusini Unguja.
Aidha aliwakumbisha wazee hao juu ya historia isiyofutika ya kijiji hicho kuwa chimbuko la masheikh wakubwa wa Zanzibar kama vile Sheikh Hassan Bin Ameir, Sheikh Fatawi Bin Issa na Sheikh Ameir Bin Tajo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Mufti,Sheikh Fadhil Soraga, ziara hiyo ya Mufti ni mfululizo wa ziara zake kutembelea wilaya zote za Unguja na Pemba .
Katika ziara hiyo alifuatana na maofisa mbali mbali wa ofisi yake pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la GNRC, Sheikh Abubakar Francis Babuogi.