Na Laylat Khalfan
Ofisa Mteule wa daraja la kwanza wa dawati la jinsia na watoto la polisi,Sajenti Zahor Faki Mjaka, amesema kumezuka mtandao wa ukahaba ambao wahusika huwapigia simu wanawake kutoka maeneo mbali mbali wakiwataka waje Zanzibar kufanya kazi za ndani, lakini baada ya kufika wanawalazimisha kufanya ukahaba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisa kwake Madema, alizitaja miongoni mwa nchi ambazo wasichana hao wanatoka kuwa ni Tanzania Bara, Kenya, Uganda na nchi nyengine jirani.
Alisema vitendo hivyo hufanywa na baadhi ya mawakala wasio waaaminifu.
Alisema mawakala wanaojihusisha kwenda mtandao huo wamekuwa wakijificha kiasi ambacho si rahisi kuwagundua.
Alisema tabia hiyo imeshamiri zaidi katika mtaa wa Mjimkongwe.
Alisema polisi wanafanya jitihada kuwabaini na kuwakamata watu hao ili kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Kwa kweli hao watu hatujawabaini kwani inaonekana wanafanya vitendo hivi kwa kujificha kiasi ambacho huwezi kuwagundua mara moja,”alisema.
Akizungumzia kuhusu vitendo vya udhalilishaji kuongezeka, alisema ni kutokana na jamii kukosa ushirikiano wa pamoja.
Alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikano wa dhati wanapoona vitendo kama hivyo vinafanyika katika mitaa yao ili kusaidia kuvidhibiti.
Alisema jina la mtandao huo unajulikana kama “help me” kwa wanawake na wanaume unajuillikana “Iga ufe”.