Na Asya Hassan, Mwashamba Juma
WIMBI la wizi wa fedha katika akaunti za wateja sasa limehamia Zanzibar, baada ya raia wawili wa kigeni kukamatwa wakihusishwa na wizi wa mamilioni ya shilingi katikia Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Raia hao wa Jamhuri ya Czec walikamatwa kwa tuhuma za wizi kwa kutumia kadi za ATM za benki hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alisema watu hao walikamatwa Agosti 19, katika maeneo ya Kwa Biziredi wakati polisi wakifanya operesheni ya kupambana na wezi wa fedha katika mabenki kwa kutumia mtandao.
Alisema baada ya kukamatwa wakiwa na ATM za benki hiyo, walifikishwa kituo cha polisi Madema kwa mahojiano.
Alisema baada ya mahojiano hayo, walizuiliwa kwa muda wa siku mbili na baadae kuachiwa kwa dhamana huku upelelezi ukiendelea.
Kuhusu matukio mengine, alisema baada ya polisi kukamilisha operesheni ya kuwalinda majaji, mahakimu na makadhi waliokutana hivi karibuni katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort, polisi wanaendelea kusimamia daftari la kudumu la wapiga kura katika Mkoa wa mjini Magharibi.
Akizungumzia ajali alisema jumla ya ajali 15 ziliripotiwa katika mkoa wa mjini magharibi na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 17.
Kuhusu gari aina ya keri, Kamanda Mkadam alisema zimeruhusiwa kubeba mizigo na si abiria na kwamba hatua zitachukulia kwa gari yoyote itakayopatikana ikibeba abiria.