Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

JK Awatunuku Nishani Maafisa, Askari JWTZ.

$
0
0
Na Mwandishi maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete, amewatunuku nishani maafisa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania baada ya kulitumikia jeshi kwa muda mrefu na kwa tabia ya kusifika.

Hafla hiyo ilifanyika jana katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga Dar es Salaam.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,Jenerali Davis Mwamunyange, aliwatunuku nishani hizo kwa niaba ya Rais.

Katika hafla hiyo maafisa na askari 147 kutoka kituo cha Upanga Dar es Salaam walivishwa nishani mbalimbali.

Nishani hizo ni ya utumishi mrefu, nishani ya utumishi mrefu na tabia njema, nishani ya utumishi uliotukuka na nishani ya ushupavu.

Msemaji wa Jeshi, Meja Erick Komba alisema nishani ya utumishi mrefu hutolewa kwa maafisa na askari wa JWTZ ambao wametimiza utumishi usiopungua miaka kumi na tano mfululizo.

Nishani ya utumishi mrefu na tabia njema huvishwa askari waliotumikia jeshi mfululizo kwa muda usiopungua miaka kumi na tano na kwa tabia ya kusifika.

Aidha alisema nishani ya utumishi uliotukuka hutolewa kwa wanajeshi wenye cheo kuanzia Meja na kuendelea ambao wametumikia jeshi kwa miaka isiyopungua ishirini mfululizo wakati nishani ya ushupavu hutolewa kwa wanajeshi waliofanya kitendo cha ujasiri.

Askari wapatao 51 ambao wamelitumikia jeshi kwa muda usiopungua miaka kumi na tano mfululizo na kwa tabia ya kusifika wamevishwa nishani ya utumishi mrefu na tabia njema, maafisa na askari 63 waliolitumikia jeshi kwa miaka isiyopungua kumi na tano wametunukiwa nishani ya utumishi mrefu, wakati maafisa wapatao 23 waliotumikia jeshi kwa muda usiopungua miaka ishirini walitunukiwa nishani ya utumishi uliotukuka wakati huo huo nishani ya ushupavu imetolewa kwa wanajeshi 10.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>