Na Tagie Daisy Mwakawago, Fatma Salum
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amependekeza Diaspora itambulike kikatiba.
Waziri Membe aliyasema hayo alipokutana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, ofisi za Tume hiyo zilizopo mjini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili suala la uraia wa nchi mbili ambalo linapiganiwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora).
“Tumekuja kuwasilisha masuala muhimu mawili; moja, uwepo wa uraia wa nchi mbili katika rasimu ya katiba na pili, katiba mpya iruhusu raia yoyote wa Tanzania aweze kuwa na uraia wa nchi nyingine pasipo kuukana uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.
Alisema wizara yake inatambua suala la uraia wa nchi mbili kuwa ni la msingi, ambalo halikugusiwa katika rasimu ya katiba iliyopo.
“Chimbuko la uraia wa nchi mbili lilitokana na wingi wa Watanzania walioko nje ya nchi ambao wanatafuta fursa ya kuwekeza na kuinua maendeleo ya nchi yao,” alisema Waziri Membe.
Aliongeza pia, “Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 inawatambua Watanzania hao na kutaka wapewe fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili katika kuinua maendeleo ya nchi.”
Alisema Watanzania hao wamekuwa wakikabiliana na matatizo kadhaa ambayo yanawanyima haki za msingi, kama vile afya, elimu na masuala ya ajira. “Kilio chao kimekuwa kero kubwa kwa vile wakati mwingine wanatibiwa kwa gharama kubwa sana ambazo hazilingani na kipato chao,” alisema Waziri Membe.
Aidha, alisema changamoto hizo zimekuwa chanzo kikubwa cha kuwashawishi Watanzania hao kuchukua uraia wa nchi za kigeni ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii kama vile elimu na afya.
“Hivi sasa sheria yetu haimruhusu Mtanzania kuchukua uraia wa nchi mbili pasipo kuukana uraia wa nchi yake,” alisema Membe, na kufafanua kuwa “Ilani ya CCM inamuhamasisha Mtanzania huyo achangie maendeleo ya nchi yake kupitia uraia wa nchi mbili.”
Waziri Membe alisema Watanzania wakiwa nje wanakosa fursa za kazi zenye kipato kikubwa wasipokuwa na uraia wa nchi hiyo, jambo linalopelekea maisha magumu na kushindwa kujikimu na kuchangia kipato chochote kwa ndugu zao walioko nchini.
“Badala yake, unakuta Watanzania wananaswa na tamaa ya ‘kujiripua’ kwa kubadili uraia wa nchi nyingine zinazokubali uraia wa nchi mbili na kuachana na uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.
Kwa upande wake, Warioba alisema maoni hayo ya uraia wa nchi mbili yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji wa maoni sehemu mbalimbali na kuongeza kuwa, hofu kubwa ya wananchi ni usalama wa nchi yao endapo uraia wa nchi mbili utaruhusiwa.
Waziri Membe alikuwa ameambatana na Balozi Gamaha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora na James Lugaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kwa upande wa Tume mbali ya Warioba, pia alikuwepo Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Salim Ahmed Salim, Mjumbe wa Tume, pamoja na Katibu Asaa Rashid na Naibu Katibu wa Tume.