Na Mwandishi wetu, Dodoma
MSWADA wa sheria wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 umepitishwa na bunge, huku Wabunge kutoka vyama vya upinzani wakisusia.Wabunge kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walitoka nje ya ukumbi wa bunge wakati Wabunge wa CCM wakipitisha mswada huo pamoja na marekebisho yake.
Wabunge wa upinzani wanapinga kwa kile wanachodai wananchi wa Zanzibar kutoshirikishwa wakati Kamati ya Bunge ya Sheria ikikusanya maoni.
Hata hivyo, licha ya mswada huo kupitishwa kulikuwa na mabishano makali kutoka kwa Wabunge wa CCM kuhusu muda wa mkutano wa bunge la katiba.
Wakati Wabunge wa upinzani wakisisitiza kuwa Zanzibar haikushirikishwa, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe,alisema maoni kutoka pande zote za muungano katika mchakato wa kubadilisha sheria hiyo yalizingatiwa.
“Katika mchakato huu ushiriki wa Zanzibar na wananchi wake ulikuwa mkubwa,” alisema Chikawe.
Alisema hakuna sheria inayosema lazima kamati ya bunge iende vituo vyote badala yake imesema mikutano inaweza kufanywa popote kati ya Dodoma, Dar es Salaam au Zanzibar.
Ili kuthibitisha hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama alimpa nafasi Mbunge wa Jimbo la Kitope, Balozi Seif Ali Iddi kulitolea kauli hilo, akiwa kama Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo,kabla ya Mhagama kumpa nafasi Balozi Seif, alisema Makamu wa Rais wa Zanzibar ni Mbunge tu na hana hakai ndani ya bunge kama Makamu wa Rais, lakini atatumia mamlaka ya kiti kumpa nafasi kuzungumzia suala hilo.
Balozi Seif alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishirikishwa kila hatua na kuliambia bunge kwamba barua iliyotumwa Serikali ya Muungano aliiandika kwa mkono wake na kutaka maneno yanayoletwa bungeni kwa njia ya panya yasichukuliwe.
Pia alitoa masikitiko na pole kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa yaliyotekea juzi bungeni.
Bunge la katiba linatarajiwa kukaa baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuandika rasimu ya pili ya katiba na katiba mpya inatarajiwa kuwa tayari Aprili 26, 2014.
Bunge limeahirishwa hadi tarehe 29 Oktoba, 2013 saa 3:00 asubuhi.