Na Mwinyi Sadallah
Wizara ya Afya Zanzibar imeruhusu mshtakiwa wa nne, Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (Jumiki), Sheikh Azzan Khalid Hamdani (56), kupelekwa nje kutibiwa baada ya kukosekana tiba ya maradhi yanayomsumbua visiwani hapa.
Sheikh Azzan alilazwa Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu baada ya kupoteza nguvu akiwa Gereza la Kiinua Miguu na imebainika anasumbuliwa na vijiwe kwenye figo.
Kuruhusiwa kwa Sheikh Azzan kupata tiba nje, kumethibitishwa na wakili wake, Salum Towfiq mbele ya Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, Yesaya Kayange.
Wakili Towfiq alisema mteja wake hali yake siyo nzuri, amepata barua ya Wizara ya Afya Zanzibar kwamba maradhi yanayomsumbua hayatibiki Zanzibar na kutaka mwongozo.
Licha ya ombi hilo, Wakili Tawfiq aliwasilisha malalamiko kuwa wateja wake wananyanyaswa, ikiwamo kutopata nafasi ya kuwasiliana na familia zao kupitia simu na wanapokuwa kwenye mazingira ya Mahakama.
Alidai Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kimewawekea utaratibu wa kukutana na familia zao mara mbili kwa mwezi, huku akiomba Mahakama itoe mwongozo.
Pia, alidai hata wanafamilia wanapotaka kwenda mahakamani kusikiliza mwenendo wa kesi hukumbana na misukosuko na kushindwa kuingia ukumbini kutokana na kuimarishwa ulinzi na kuzuia njia za kuingia na kutoka.
Hata hivyo, Kayange alisema ombi la kwanza la matibabu ya mshtakiwa liko nje ya uwezo wake na kutaka liwasilishwe Mahakama Kuu. Pia, katika ombi la pili alikitaka Chuo cha Mafunzo Zanzibar kuwatendea haki washtakiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria. Kayange aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 7.
Chanzo - Mwananchi